2017-05-24 07:45:00

Ni mauaji ya kinyama dhidi ya watu wasiokuwa na hatia!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anaonesha kusikitika sana kutokana na mauaji yaliyotokea huko Manchester, Uingereza usiku wa kuamkia Jumanne, tarehe 23 Mei 2017 na kusababisha  vijana na watoto 22 kupoteza maisha na wengine 59 kujeruhiwa vibaya baada ya kutokea shambulizi la kigaidi kwenye Uwanja wa Manchester ambako mwanamuziki Ariana Grande alikuwa anatumbuiza umati mkubwa wa vijana.

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wale wote walioguswa na kutikiswa na shambulizi hili la kikatili. Anapenda kuwatia shime wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto waliojeruhiwa pamoja na kutoa faraja kwa familia zinazoomboleza kwa kuondokewa na wapendwa wao! Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia wote hawa baraka zake za kitume katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo!

Wakati huo huo, Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles anasema, amesikitishwa sana na shambulizi hili la kigaidi dhidi ya vijana na watoto wasiokuwa na hatia. Anapenda kwa niaba ya Kanisa Katoliki nchini Uingereza kuungana na waombolezaji wote, ili kusali kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliofariki dunia pumziko la milele na majeruhi waweze kupata nafuu na hatimaye, kurejea tena katika shughuli zao za kila siku. Kanisa linawashukuru wote waliosaidia mchakato wa kuwaokoa watoto waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa michezo wa Machester, Uingereza. Kardinali Nichols katika ujumbe wake kwa Askofu John Arnold wa Jimbo Katoliki Salford ambamo kuna Uwanja wa Michezo wa Manchester, anaombea toba na wongofu wa ndani wale wote walioshiriki kupanga na kutekeleza shambulio hili la kigaidi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia. Wanawaombea ili hatimaye, waweze kutambua mpango wa Mungu katika historia na maisha ya binadamu.

Naye Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia anasema, familia ya Mungu Barani Asia inapenda kuungana na wale wote wanaoomboleza kwa kuondokewa na wapendwa wao! Wanawaombea majeruhi kupona haraka iwezekanavyo. Kardinali Gracias anasema, kwa maombezi ya Bikira wa Fatima, amani iweze kuchipua tena katika nyoyo na akili za watu; ili kuweza kupambana na ubaya, hatimaye, wema na amani viweze kutawala duniani. Kardinali Oswald Gracias anaombea wongofu wa ndani ili kuondokana na utamaduni wa kifo unaoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Anawataka waamini kamwe wasikate tamaa kuombea amani duniani, kwa kutambua kwamba amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na iko siku amani itaweza kutawala duniani!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Eamon Martin kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Ireland anapenda kutuma salam zake za rambi rambi kwa familia zilizopatwa na msiba huo mkubwa, changamoto ni kwa watu wote kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa haki, amani, upendo, matumaini na mshikamano wa dhati duniani! Shambulizi hili la kigaidi limelaaniwa pia na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa  na kwamba, kuna haja ya kushikamana kwa dhati ili kukomesha vitendo vya kigaidi duniani vinavyoendelea kupandikiza mbegu ya hofu na utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.