2017-05-23 15:55:00

Dhamana na wajibu wa mihimili ya uinjilishaji ndani ya Kanisa!


Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mongomo nchini Equatorial Guinea ina mshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuipatia mchungaji mkuu wa kwanza Askofu Juan Domingo-Beka Esono Ayang ambaye amepewa dhamana ya kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Haya ni matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki Equatorial Guinea kuanzia mwaka 2011 lilipofanya hija yake ya kitume mjini Vatican. Lengo lilikuwa ni kusogeza huduma ya kichungaji kwa familia ya Mungu na hatimaye, kukoleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kuhakikisha kwamba, waamini wanapata majiundo awali na endelevu katika maisha na tunu msingi za Kikristo, tayari kuzitolea ushuhuda sanjari na kukabiliana na changamoto mamboleo!

Haya yamesemwa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu alipokutana na kuzungumza Wakleri pamoja na watawa wanaofanya utume wao Jimboni Mongomo, Equatorial Guinea, Jumatatu, tarehe 22 Mei 2017.  Jimbo Katoliki la Mongomo ni kielelezo cha Kanisa linaloendelea kukua na kukomaa, tayari kupyaishwa kwa Injili na utume, changamoto inayohitaji kweli watu wa sifa watakaojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa.

Mihimili ya uinjilishaji ina dhamana ya kusaidia ukuaji na ukomavu wa imani ya familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo. Huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimissionari, tayari kujikita katika utakatifu wa maisha, huduma ya upendo na mshikamano wa dhati kwa watu wa Mungu. Mihimili yote ya uinjilishaji inahamasishwa na Mama Kanisa kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaojikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili zinazofumbatwa katika: utii, ufukara na useja. Wajitahidi kupenda kama ambavyo Kristo mwenyewe anawapenda watu wake; kufikiri na kutenda kama Kristo mwenyewe aliyekuja si kuhudumiwa bali kuhudumia na kuyatoa maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi. Kardinali Filoni anakaza kusema, utambulisho wa wakleri na watawa unapaswa kusimikwa katika: maisha ya sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa kwa Ibada na uchaji. Wawe ni watu wa imani wanaotegemea ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao na wala si vinginevyo, kwani kinyume cha hapo ni ubatili mtupu!

Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mongomo inawajibika kujiwekea sera na mikakati ya maendeleo: kiroho na kimwili na kuhakikisha kwamba, waamini wote kadiri ya dhamana, nafasi na uwezo wake wanachangia kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia. Waamini wajenge upendo wa dhati kwa Jimbo lao na hivyo kuwa tayari kulitegemeza kwa hali na mali! Kwa vile mapadre ni wasaidizi wa kwanza wa Askofu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, kumbe, hawana budi kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali nguvu, akili, ujuzi na maarifa katika kutekeleza mipango ya shughuli za kichungaji na maendeleo ya Jimbo lao. Mapadre na watawa wanahamasishwa kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa kwa familia ya Mungu Jimboni Mongomo. Hakuna jambo linalotesa na kusumbua sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kama dhambi na makawazo yanayofanywa na wakleri na watawa ndani ya Kanisa! Badala ya kuwa wachungaji wema, wanabadilika kuwa ni mafisadi na wanyang’anyi wa kondoo wa Kristo, kiasi cha kujikuta wanatumbukia katika mtandao wa dhambi ya mauti.

Ukosefu wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni kikwazo kikubwa kwa familia ya Mungu; ukabila, ubinafsi, uchoyo na uchu wa mali na madaraka ni sumu kubwa katika ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia. Ukosefu wa heshima, nidhamu na utii kwa Askofu mahalia; hali ya kutowajali na kuwathamini waamini walei, ni hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya Jimbo. Mapadre na watawa wanapaswa kuwa ni kielelezo cha Kristo mchungaji mwema; mashuhuda amini na wenye mvuto wa Kristo Yesu ambaye ni: fukara, mtii na msafi kamili!

Mapadre waendelee kujitakasa wanapoadhimisha Mafumbo ya Kanisa, ili kuwa kweli ni viongozi wenye nguvu ya kimaadili na utu wema, watu wanaoweza kusikilizwa na kuthaminiwa na wale wanaowazunguka! Mapadre na watawa wajitahidi kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili katika maisha na utume wao; kwa kuwa ni watu wenye kiasi, wasiovurugwa na malimwengu, anasa na utajiri wa duniani! Waoneshe upendo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu, daima wakiwa tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Uongozi ndani ya Kanisa utambulike kuwa ni huduma kwa ajili ya familia ya Mungu!

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anaitaka mihimili ya uinjilishaji mpya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa maisha, kwa kutambua kwamba, kimsingi Kanisa ni la kimissionari na kwamba, linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Kanisa linakuwa na kupanuka kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala si kwa njia ya ncha ya upanga au mtutu wa bunduki! Ushuhuda huu unajikita katika maisha ya kiroho, kimaadili na kichungaji! Mapadre wanahimizwa na Baba Mtakatifu Francisko kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Upadre ni wito na zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Kanisa na wala si kazi ya mshahara. Mwishoni, Kardinali Filoni, anaitaka mihimili yote ya uinjilishaji, kuungana, kushikamana na kutembea pamoja na katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji Jimboni mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.