2017-05-22 15:27:00

Watoto wa Parokia ya Pier Damiani wamweka "kiti moto" Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jumapili ya ya VI ya Kipindi cha Pasaka, tarehe 21 Mei 2017 ametembelea na kusali kwenye Parokia ya Pier Damiani iliyoko kwenye Jimbo kuu la Roma. Amepata nafasi ya kuzungumza na watoto wanaojiandaa kupokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza katika maisha na kujibu maswali mawili ya msingi. Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wagonjwa Parokiani hapo; Jumuiya ya Ukatekumeni Mpya pamoja na maskini wanaohudumiwa na Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki Italia, Caritas. Baba Mtakatifu amepata pia nafasi ya kutoa Sakramenti ya kitubio kwa waamini wanne na baadaye ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.

Watoto wamemuuliza Baba Mtakatifu kadiri ya umri na uwezo wao, Je, wanaweza kufanya nini ili kuwaokoa watoto wengine wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia? Wamemuulizia jinsi ambavyo aliweza kutambua wito wa Daraja Takatifu ya Upadre? Je, wao kama watoto wanawezaje, kumfuasa Kristo Yesu kwa ukamilifu zaidi na mwishoni, watoto hawa katika udadisi wao, wamemuulizia Baba Mtakatifu Francisko ni mchezo gani alikuwa anapenda kushiriki alipokuwa mtoto mdogo mwenye umri kama wao! Watoto wameshiriki  kujibu swali la msingi kwa kusema kwamba, hata wao wanaweza kushiriki katika kazi ya ukombozi wa watoto wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya sala na sadaka yao nyofu! Watoto wanaweza kuendeleza dhamana hii kwa kuwaheshimu watu wote; wakubwa kwa wadogo; wazee kwa vijana; maskini kwa matajiri; kwa maadui na marafiki! Kwa kusamehe na kusahau, ili kuanza kuandika upya ukurasa wa maisha!

Watoto wanaweza kushiriki katika ukombozi wa watoto wenzao kwa kutoshirikiana na watu wabaya. Hivi ndivyo hata watoto wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika machakato wa kazi ya ukombozi wa mwanadamu. Watoto wawe na ujasiri wa kufikiri na kutenda mema; kusali na kucheza kwa juhudi na maarifa; ili kuweza kushirikishana furaha ya Injili na wale wanaojisikia kuwa wapweke. Katika utoto wake anasema Baba Mtakatifu alipenda kucheza mpira wa miguu, lakini anakiri kwamba, alikuwa ni miguu mizito kiasi cha kushindwa kutandaza vyema kabumbu na kwamba, alipenda kuwa ni mlinda mlango!

Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu anamwita kila mwamini kwa wito, kazi na dhamana maalum ndani ya Kanisa na katika Jamii. Yesu anataka baadhi ya waamini waweze kufunga ndoa na kuzaa watoto, tayari kujenga na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani! Anawataka baadhi ya vijana waweze kujisadaka katika maisha na wito wa Kipadre ili kuwatakatifuza, kuwaongoza na kuwafundisha watu wa Mungu. Wengine wanaitwa kuwa ni watawa ili kujisadaka katika maisha ya sala na huduma kwa Mungu na jirani. Sehemu kubwa ya waamini ni walei ambao wanahamasishwa na Mama Kanisa kujenga na kudumisha familia bora za Kikristo. Anawataka watu wafanye kazi ili waweze kupata riziki yao ya kila siku. Wao katika familia yao walikuwa ni watoto watano waliokuwa na furaha na walipenda kucheza sana. Lakini siku moja, kidogo, Kaka yao mkubwa apoteze maisha kwa kucheza mchezo wa hatari. Wazazi wao waliwasaidia kwenda shule na daima walijitahidi kuwapatia ulinzi na tunza.

Kumbe, inapendeza kuona mwanaume na mwanamke wanaooana na hatimaye, kupata watoto ambazo ni zawadi kubwa kwa Mwenyezi Mungu, huku wakiwa tayari kuwatunza na kuwaelimisha. Ni jambo jema kuwa na wito wa kifamilia ili kuunda familia! Watoto wamewashukuru na kuwapongeza wazazi wao wanaojisadaka kwa hali na mali ili kuhakikisha ustawi na maendeleo yao: kiroho Na kimwili. Inapenda pia kwa vijana kuwa Mapadre na Watawa. Akiwa na umri wa miaka 16 alijisikia ndani mwake wito wa kuwa Padre, na leo hii anamshukuru Munngu kwamba, amebahatika kuwa Padre. Hivi ndivyo inavyotokea hata kwa vijana kuanza kuchumbiana na hatimaye kufunga Ndoa. Watoto wawaheshimu na kuwatii wazazi na walezi wao, kwani wao wanajisadaka kwa ajili ya maendeleo yao ya kila siku. Mwishoni, walisali na kuombeana na hatimaye, akawapatia baraka yake ya kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.