2017-05-22 15:06:00

Papa Francisko anawataka waamini kumfungilia Roho Mtakatifu nyoyo zao


Injili ya Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka imejikita katika wosia wa Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kabla ya kupaa kwenda mbinguni kwa Baba yake. Yesu anawataka wafuasi wake kushika Amri zake naye atawaombea kwa Baba yake wa mbinguni Msaidizi mwingine, ndiye Roho wa kweli, anayekaa kwao na atakuwa ndani mwao. Huyu ndiye Roho Mtakatifu ambaye waamini wanampokea wakati wa Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. Ndiye Roho anaye walinda na kuwategemeza ili kweli wasibaki yatima!

Waamini wanaalikwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko ndani mwao anatembea pamoja nao; anawaonesha dira na mwongozo wa kufuata; anawapatia nguvu na ujasiri wa kupambana na vishawishi katika maisha, kwani huyu ni Wakili mwema na mwaminifu. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini  kusali na kumwabudu Kristo Yesu anayekaa katika nyoyo zao. Wakristo wanapaswa kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililoko ndani mwao, kwa njia ya upole na kwa hofu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 21 Mei 2017, kwenye Ibada ya Misa Takatifu, wakati wa hija yake ya kitume kwenye Parokia ya Mtakatifu Pier  Damiani, Jimbo kuu la Roma. Katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee, dhamana na kazi ya Roho Mtakatifu miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Waamini waoneshe na kushuhudia tumaini liliko ndani mwao kwa njia ya upole na hofu ya Mungu katika maisha yao; tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Hofu na upole vinabubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu, ili kuwasaidia waamini kuwaheshimu na kuwathamini jirani zao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwovu shetani anafahamu mbinu mbali mbali za kuwakwamisha waamini katika huduma kwa Mungu na jirani. Anawakosesha kwanza kabisa moyo wa upole na hofu ya Mungu, kiasi cha kuwavuruga na kuwasambaratisha kama Jumuiya ya Wakristo. Waamini wajitahidi kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu wa ndani kwa kujikita katika upole na hofu ya Mungu; kwa kuondokana na “majungu yasiyokuwa ni mtaji” pamoja na kuondokana na kinzani na mipasuko ya kidini. Waamini wahakikishe kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Roho Mtakatifu ndani mwao, ili kuondokana na chachu ya wivu usiokuwa na mashiko; uchu na tamaa ya madaraka; mambo yanayowagawa watu na kuharibu msingi wa umoja, ushirikiano na mapendo.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni tema ambayo kimsingi ni changamoto kwa Jumuiya nyingi za Kikristo. Wakati alipokuwa anafukizia ubani kwa Sanamu ya Bikira Maria, Mkingiwa Dhambi ya Asili, chini yake alimwona yule nyoka aliyepondwa kichwa, akiwa mdomo wazi na ndimi zikiwa nje. Kwa wale Wakristo wasiomtunza Roho Mtakatifu ndani mwao kwa upole na hofu ya Mungu ni watu “wenye midomo mirefu”, wanaoweza kukomunika hata wakiwa mlangoni pa Kanisa hata kabla ya kujongea Altareni”.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ndio ukweli “Umbeya, chuki na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko ni mambo yanayobomoa Jumuiya za Kikristo. Kwa waamini wanaojisikia kuwa na “mdomo mrefu” wanapaswa kumwomba Bikira Maria ili awasaidie kupambana na mwovu shetani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Roho Mtakatifu anayeishi ndani mwao, kama alivyofanya Yeye mwenyewe na hatimaye akabahatika kuchukua mimba na kumzaa Mwana wa Baba wa milele. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujitahidi kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na kamwe wasimpatie shetani nafasi kwani atawachezesha “rumba” ya kukata na shoka kiasi hata cha kusambaratika. Waamini wajitahidi kutomhuzunisha Roho Mtakatifu anayekaa ndani mwao, bali wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa: heshima, upole na hofu ya Mungu kwa jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.