2017-05-20 13:36:00

RENAMO inataka kuandika ukurasa wa amani nchini Msumbiji!


Kwa miaka mingi familia ya Mungu nchini Msumbiji imekuwa ikiishi kwa hofu na mashaka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, iliyokuwa inaendeshwa kati ya Chama tawala cha FRELIMO kilichoko madarakani na Chama cha upinzani cha RENAMO. Bwana Alfonso Dhlakama, ndiye kiongozi mkuu wa RENAMO ambaye kuanzia mwaka 1976 Msumbiji ilipojipatia uhuru wake amekuwa akiendesha vita ya wenyewe kwa wenyewe, hadi mwaka 1992, Msumbiji ilipotia sahihi kwenye Mkabata wa amani na hapo wananchi wakaanza kuwa na matumaini ya Msumbiji yenye amani, tayari kucharuka katika mchakato wa maendeleo endelevu!

RENAMO kikageuka kuwa ni Chama cha upinzani na kuanza pilika pilika za kuwania uongozi wa nchi. Lakini hakijawahi kufanikiwa kutwaa madaraka na kuongoza nchi! Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, uchu wa madaraka ulivuruga RENAMO ikakataa kukubali kushindwa kwenye chaguzi kuu za Rais na Wabunge na hatimaye, kurejea tena msituni kutaka kushika madaraka kwa njia ya mtutu wa bunduki! Kuanzia mwaka 2014 kumekuwepo na mchakato wa majadiliano na FRELIMO ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, jambo ambalo halikufua dafu kwa FRELIMO, ikakaza kamba kutaka demokrasia na utawala wa sheria kuheshimiwa na wote!

Hivi karibuni, Bwana Alfonso Dhlakama, kiongozi mkuu wa RENAMO ametangaza rasmi kwamba, RENAMO imeachana na sera za kutumia mtutu wa bunduki kutaka kuingia madarakani na kwamba, huu ni mwanzo mpya wa maisha ya wananchi wa Msumbiji, baada ya kuteseka kwa miaka 40 ya vita na mashambulizi ya kushtukiza. Hii ni habari njema na yenye kuleta matumaini katika mchakato wa maendeleo endelevu ya wananchi wa Msumbiji, kwani amani ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu! Wananchi wa Msumbiji wanasema, wamechoka kusikia maneno matupu ambayo hayavunji mfupa, sasa wanataka kuona amani ikitekelezwa kwa vitendo kwa kuhakikisha kwamba, yale mambo msingi yaliyokubaliwa kwenye mikataba ya amani kwa juhudi za usuluishi wa kimataifa na kitaifa inatekelezwa kwa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.