2017-05-19 09:30:00

Sherehe ya Ekaristi Takatifu kuadhimishwa Jimboni Roma, Jumapili


Kwa mara ya kwanza katika historia, Jimbo kuu la Roma litaadhimisha Siku kuu ya Ekaristi Takatifu Jumapili tarehe 18 Juni 2017 baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuridhia mabadiliko haya yanayolenga kuwapatia waamini wengi zaidi nafasi ya kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu na hatimaye, kuweza kuandamana na Yesu wa Ekaristi katika viunga vya Jimbo kuu la Roma. Kwa Makanisa mahalia, Siku kuu ya Ekaristi Takatifu inaadhimishwa Jumapili kwa Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kufuatiwa na maandamano makubwa, ushuhuda wa hadhara wa Sakramenti kuu: kielelezo cha Karamu ya Pasaka yaani sadaka ya Kristo Msalabani; alama ya shukrani, kumbu kumbu endelevu na uwepo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai!

Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu Jimbo kuu la Roma kama kawaida yataadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kuanzia saa 1:00 za Usiku kwa Saa za Ulaya na kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, kufuatiwa maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kuelekea kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma. Hapo Baba Mtakatifu atatoa baraka kuu ya Ekaristi Takatifu. Taarifa hii kwa vyombo vya habari imetolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Wakati huo huo, Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa anasema, ratiba elekezi ya maadhimisho ya Ibada zitakazoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Juni 2017 inaonesha kwamba, Papa ataongoza Ibada ya Siku kuu ya Pentekoste, tarehe 4 Juni 2017, Kanisa linapokumbuka Siku ile lilipozaliwa rasmi na Mitume wakatoka kifua mbele kutangaza kwa ujasiri kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ni Siku ya Waamini walei wanaohamasishwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya matendo yenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji!

Tarehe 29 Juni 2017, saa 3: 30 asubuhi kwa saa za Ulaya, Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo mitume; miamba wa imani, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kubariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu walioteuliwa na Baba Mtakatifu katika kipindi cha Mwaka 2016 – 2017. Kutokana na utaratibu mpya, Maaskofu wakuu watavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika, ili kuwapatia nafasi waamini wa Majimbo makuu kushiriki katika Ibada hii, kama kielelezo cha mshikamano wa Kanisa mahalia na Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.