2017-05-17 15:26:00

Dhamana na wajibu wa Roho Mtakatifu katika maisha ya waamini!


Ndugu wapendwa, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka inaongozwa hasa zaidi katika Injili na NENO KUPENDA au UPENDO. Hivi unajisikiaje unapoambiwa nakupenda au unapohisi kuwa unapendwa? Hakika kupenda kunawajibisha na tamko hilo husubiri jibu. Wengi wetu twafahamu fika jinsi ilivyo vigumu kupenda upeo. Upendo unadai matendo. Kinachofuata ni wajibu. Ndicho tulichosikia Jumapili iliyopita – ushuhuda na utumishi. Yule anayempenda Mungu hana budi kumtumikia. Ndio wito unaoonekana katika masomo yetu ya leo = kutii amri na kuabudu. Ndiyo maana Yesu anaweza kusema mkinipenda mtazishika amri zangu. Mt. Tomas wa Aguino anasema sheria za Mungu ni nyepesi kwa wapendao na mzigo kwa wasiopenda.

Katika 1Yoh.4,8 tunasoma, yeye asiyependa hakumjua Mungu kwa maana Mungu ni upendo. Kwa maana hii ili kupenda vizuri ni lazima kumjua Mungu sababu yeye ni PENDO. Mapendo ya kweli yadai sadaka. Ili kushika amri au sheria inavyotakiwa yahitaji sadaka kubwa na inayodai utumishi. Tunakumbushwa kuwa huwezi kupenda bila kutoa. Oneni jinsi Mungu alivyotupenda sisi hata akamtoa mwanae wa pekee atukumboe.  Mtakatifu Augustino anapotafakari juu ya upendo wa Mungu anasema - umegusa mioyo yetu kwa pinde za upendo wako na akili zetu kwa mishale ya neno lako. Katika somo la kwanza, tunaona jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi ndani ya Petro. Ubatizo wetu unatuwajibisha. Sisi tumebatizwa kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tumezamishwa ndani yake Mungu, katika Utatu Mtakatifu. Sisi tunashiriki ile asili ya Kimungu. Hatuitwi kwa jina lingine ila ni watoto wa Mungu na ndivyo tulivyo.

Katika somo la pili, twaona wingi wa neema ya tendo la Mungu la kuokoa na hitaji la utayari wa mkristo. Petro anasema mpokeeni Kristo, na ondoeni roho ya woga. Halafu Petro asema - kuweni na uwezo wa kuelezea imani yenu - ni kwa ajili yake twafanya mambo haya. Imani yetu na maisha yetu - msingi wake ni Kristo aliyekufa na kufufuka. Sababu ya matumaini yetu inaonekana katika ukuaji wa ufalme wa Mungu na kumpenda Mungu. Matumaini yetu ni ufalme wa Mungu, utukufu wa Mungu, upendo wake, ujio wa mbingu mpya na nchi mpya, ujio wa ufalme wa haki na amani. Tukumbuke kuwa Roho wa Mungu hushuhudiwa na anatakiwa aonekane katika maisha yetu ya kila siku. Katika Gal. 5:22-23 – tunatafakarishwa na matokeo ya Roho - lakini matokeo ya Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, hisani, ukarimu, uaminifu, upole na kiasi.

Katika somo la Injili tunasikia kuwa Baba atawapatia Roho Mtakatifu. Hivyo tunamwona Baba anayependa kwa njia ya Roho Mtakatifu na Mwanaye. Katika upendo huo wa Roho Mtakatifu, Petro na Yohani wanaondoka kwenda kutangaza habari njema na wale waliobatizwa na Filipi wakawekewa mikono na kupokea Roho Mtakatifu. Na hapo yaonekana mwanzo wa mitume kwenda kuhubiri habari njema duniani. Ndiyo maana sisi tumeitwa kuitikia huu mwito ni kuishi kadiri ya amri za Mungu. Mambo haya mawili hayatengani - upendo na utii.

Huyu Roho anayepelekwa atawezesha udumifu wetu katika maisha ya ukristo. Huyo Roho ni wakili, mfariji, mshauri, msaidizi. Na hii ndiyo kazi kuu ya Roho Mtakatifu. Katika maana ya Kigriki, roho ni yule anayesimama kando ya mteja na kwa lugha ya kisheria ni mwanasheria, wakili. Pengine katika lugha ya siku hizi tungesema ni kocha, mwalimu. Roho Mtakatifu yupo nasi pamoja na anatuongoza. Twaweza kujiuliza kwanini twahitaji huyu Roho Mtakatifu? Majibu yako mengi; Hakuna mwanadamu aliye mkamilifu; Mganga hajigangi; Hata wachezaji maarufu – mpira, mbio, wanamuziki, watu maarufu wa masiha ya kiroho n.k wanahitaji mwalimu. Peke yetu bila Mungu hatuwezi kitu. Watu wengi huamini na kudhani kuwa hawana haja ya msaada, ushauri, mawaidha, kushirikiana na wengine n.k. Je ni kweli?

Katika mojawapo ya mafundisho ya Kardinal Ratzinger (Papa Benedict XVI) kabla ya uteuzi, akiongea dhidi ya watu wanaoishi bila mwelekeo, anasema kuwa wanaodhani hawamhitaji Mungu na mwanadamu mwenzio, matokeo yake huwa kinyume cha wote. Ndugu zangu ili tuweze kupokea hiyo zawadi ya Mungu, huyo Roho Mtakatifu, hatuna budi kuishi amri ya mapendo kwa Mungu na jirani -  Yoh 14,15-16 Ndugu zangu, jumapili ijayo tutaadhimisha sherehe ya Kupaa Bwana. Baada ya Kupaa Bwana, mitume na wanawake walienda chumba cha juu – wakisali na kusubiri - Mdo 1,14,  hatuna budi nasi kufanya hivyo. Kipindi kati ya kupaa Bwana na Pentekoste ni kipindi cha sala na subira - tukijiandaa kumpokea Roho Mtakatifu. Sote tunaalikwa kufanya hivyo - tunamhitaji mwalimu, kiongozi n.k leo kama iliyokuwa miaka 2000 iliyopita.

Mungu ametupa pendo na amri - sisi tumetoa nini?

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.