2017-05-16 15:45:00

Papa Francisko: Rais Macron: Jengeni jamii yenye haki na udugu!


Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za pongezi na matashi mema Bwana Emmanuel Macron, Rais mpya wa Ufaransa baada ya kuapishwa rasmi, Jumapili, tarehe 14 Mei 2016 huko Paris, Ufaransa. Baba Mtakatifu anamwombea Rais Macron kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumwinua katika utumishi wake ili Ufaransa ikidumu katika uaminifu wake katika utajiri wa utofauti wao; mapokeo yao ya kimaadili sanjari na amana ya maisha ya kiroho inayopambwa kwa Mapokeo ya Kikristo, iweze kujielekeza zaidi katika ujenzi wa wa jamii ambayo inasimikwa katika haki na udugu!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Rais wa Ufaransa ataendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa utofauti na kuwaangalia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa jicho la pekee, ili hata wao pia waweze kushiriki katika ujenzi wa mshikamano kati ya watu wa mataifa. Ufaransa iendelee kujizatiti zaidi Barani Ulaya na katika ulimwengu kutafuta amani na mafao ya wengi; kwa kuheshimu na kuenzi maisha na utu wa binadamu na watu wote. Mwishoni, Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu kwa moyo wake wote, ili aweze kumbariki Rais mpya pamoja na wananchi wote wa Ufaransa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.