2017-05-15 09:24:00

Papa Francisko achonga na wanahabari na kukazia: matumaini na amani!


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017 amehitimisha hija yake ya 19 ya kitume nchini Ureno ambako ameshiriki katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. Hija hii imeongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mjini Fatima 2017 pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”. Akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, Baba Mtakatifu amemkabidhi Bikira Maria mateso, mahangaiko na matumaini ya familia ya Mungu. Amewatangaza Wenyeheri Francis Marto na Yacinta Marto kuwa ni watakatifu, mfano bora wa kuigwa katika maisha ya Kikristo kwa kutambua uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na watu; kwa kudumu katika sala, toba, wongofu wa ndani; kwa kutimiza malipizi ya dhambi za walimwengu pamoja na kuendelea kuombea amani duniani!

Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican, kama kawaida alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, amewashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi cha masaa 24 ili kuwajuza watu wa Mataifa kile kilichokuwa kinajiri katika hija yake ya kitume kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima. Baba Mtakatifu anakaza kwa kusema, hija yake nchini Ureno imekuwa ni hija ya matumaini na amani duniani! Huu ni ujumbe wa Bikira Maria ambao aliwadhaminisha Watoto watatu wa Fatima yaani: Mtakatifu Francis Marto, Mtakatifu Yacinta Marto na Mtumishi wa Mungu Lucia dos Santos. Kutangazwa kwa Watakatifu Francis na Yacinta Marto anasema Baba Mtakatifu imekuwa ni furaha kubwa ya matumaini na amani duniani!

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 24 Mei 2017 mapema majira ya asubuhi anatarajia kukutana na kuzungumza na Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye katika sera na mikakati yake ya kisiasa na kiuchumi anaendelea kujielekeza katika ujenzi wa kuta za utengano; kutojali kilio cha wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi na kwamba, anaendelea kuangalia uwezekano wa kutotekeleza Itifaki ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kama ilivyotiwa mkwaju na Jumuiya ya Kimataifa kwa shida na taabu kubwa.

Baba Mtakatifu anasema, kwa upande wake, atasema kile ambacho kimefumbatwa katika sakafu ya moyo wake na kwamba, si utamaduni wake kumhukumu mtu hata kabla ya kumsikiliza! Maisha ya mwanadamu yanaendelea daima kuwa ni fumbo, lenye milango wazi, changamoto ni kutafuta milango ambayo bado ni wazi, ili kuweza kuzungumza kuhusu mafao ya wengi na kusonga mbele kwa matumaini zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amani ni sanaa inayopaswa kufanyiwa kazi hatua kwa hatua na kwamba, mambo mazuri hayana haraka. Utamaduni wa amani unajengwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana.

Baba Mtakatifu akizungumzia kuhusu “Udugu wa Mtakatifu Pio X” ambao una ibada maalum kwa Bikira Maria wa Fatima anasema, kimsingi, ana uhusiano mzuri na Askofu Fellay na kwamba, wamekuwa wakizungumza pamoja mara kwa mara. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hapendi kufanya mambo kwa haraka haraka kwani hayana baraka, bali pole pole ndiyo mwendo, unaowaunganisha watu katika hija ya pamoja, ili hatimaye, kufanya maamuzi ya busara. Hapa hakuna mshindi wala aliyebwagwa na kugalagazwa, bali hapa kuna tatizo na ndugu katika Kristo wanaopaswa kutembea kwa pamoja kama ndugu! Kumbe, hapa kunatakiwa kuwa ni formula itakayotumika, ili wote kwa pamoja waweze kutembea kwa kushikamana mikono!

Majadiliano ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa! Haya ni majadiliano ya kidini na kiekumene; kitamaduni na kidiplomasia. Kumekuwepo na mwelekeo mzuri wa majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Kipentekoste. Huu ni uekumene unaofumbatwa katika sala, maisha ya kiroho; ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakristo kwa pamoja wanataka kutangaza na kushuhudia Injili ya amani, huruma na upendo kwani wanatambua kwamba, Kristo Yesu ni Bwana na Mkombozi wa dunia; ni chemchemi ya neema na baraka kwa watu wake!

Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Fatima, miaka 25 iliyopita, Baba Mtakatifu Francisko aliteuliwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina, huo ukawa ni mwanzo mpya wa historia, maisha na utume wake. Anakiri kwamba, tukio hili hakuwa amelipatia uzito wa pekee sana, lakini wakati alipokuwa anasali mbele ya Bikira Maria wa Fatima, alimgusia tukio hili na kumwomba amwombee: huruma na msamaha kutokana na mapungufu na dhambi ambazo ametenda katika kipindi chote hiki. Nchini Italia kuna kashfa ambayo imeibuliwa hivi karibuni kwamba, kuna baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanashirikiana na baadhi ya wafanyabiashara haramu ya binadamu inayowahusisha wakimbizi na wahamiaji kutoka Kaskazini mwa Afrika. Hapa Baba Mtakatifu anasema, amefuatilia sakata hili, lakini bado anavuta subira ili kufahamu hatima yake kabla ya kutoa maoni yake binafsi!

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, yamekuwa ni ushuhuda wa imani na Ibada kwa Bikira Maria, kutoka kwa watu mbali mbali duniani! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwake, Ibada safi ya Bikira Maria inajikita katika utambuzi kwamba, ni Mama wa Mungu, Mama wa Kanisa na Mama wa wote na wala si mfanyakazi wa Posta ambaye kila mwezi anatuma notisi kwa watu. Kwa hakika huyu si Mama wa Yesu! Lakini, kwa upande mwingine wa shilingi anasema Baba Mtakatifu Medjugorie kuna mwelekeo wa maisha ya kiroho na kichungaji unaopaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa!

Tayari changamoto hii iliwahi kufanyiwa kazi na Papa Mstaafu Benedikto XVI kwa kuunda Tume ya Kardinali Ruini. Hapa kuna watu wanaokwenda kusali, watu wanaotubu na kumwongokea Mungu; hapa kuna watu wanaokutana na Mungu katika maisha yao! Kumbe, kuna haja ya kulichukulia suala hili katika uzito wake wa kichungaji, changamoto ambayo imevaliwa njuga kwa sasa na Askofu ambaye baadaye, atatoa maoni na hatimaye, Kanisa kuchukua uamuzi wa kudumu.

Kuhusu sakata la Mary Collins kung’atuka kutoka katika Tume ya Kipapa ya ulinzi wa watoto wadogo anasema, amezungumza kwa kina na mapana na Mama huyu na kwamba anaendelea kushirikiana na tume kutoka nje, kwa ajili ya kuwafunda Wakleri kuhusu tema hii. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu huyu ni mwanamke wa shoka anataka kuchakarika na kuona matunda ya kazi zao! Shutuma zake ni kweli kwani kuna kesi ambazo zimecheleweshwa sana kutolewa maamuzi. Hii inatokana na upungufu wa rasilimali watu wanaoweza kutekeleza dhamana hii kwa haraka na kwa umakini mkubwa. Kuna zaidi kesi elfu mbili zinazopaswa kufanyiwa maamuzi katika ukweli, uwazi na haki!

Kuhusu swali la ukanimungu na utopeaji wa imani katika nchi ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikijulikana kama nchi za Kikatoliki duniani, Baba Mtakatifu Francisko anasema, hili ni tatizo na changamoto inayomsumbua sana moyoni mwake. Kuna nchi nyingi ambazo ni za Kikatoliki, lakini ni wapinzani wakubwa wa Kanisa! Kumbe, kuna haja kwa Wakleri kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, ili kuendelea kuwa karibu zaidi na watu wa familia ya Mungu! Upadre ukigeuzwa kuwa kama kazi ya mshahara, hapa kuna hatari ya Kanisa kukumbukwa na saratani kubwa ya kukimbiwa na waamini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.