2017-05-13 15:45:00

Sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Bikira Maria wa Fatima!


Baba Mtakatifu Francisko kama mahujaji wengine wote wanaokwenda kuhiji kwenye Madhabahu ya Fatima, Ijumaa jioni, tarehe 12 Mei 2017 alitembelea Kikanisa cha Tokeo la Bikira Maria wa Fatima na kusali kwa kitambo kirefu mbele ya Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima na hatimaye kuweka shada la maua ya dhahabu mbele ya sanamu. Baba Mtakatifu katika sala yake kwa Bikira Maria wa Fatima, ameombea: matumaini, amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anamshukuru Bikira Maria wa Fatima, Mama mwenye Moyo Safi usiokuwa na doa, kimbilio na njia inayowaongoza watu kwa Mwenyezi Mungu, anamshukuru kwani yuko mbele yake kama hujaji wa matumaini na amani; anapenda kuombea maridhiano kati ya watu! Yuko mbele yake kama Nabii na mjumbe wa huduma inayowaunganisha wote!

Baba Mtakatifu anamsalimia Bikira Maria ambaye miaka 100 iliyopita ameonesha mpango wa huruma ya Mungu, yuko mbele yake kama waamini wote wanaong’aa kwa mavazi meupe ya ubatizo, ili kuishi ndani ya Mwenyezi Mungu kwa kusali kwa ajili ya kuombea amani! Anamkimbilia Bikira Maria hujaji, Malkia; Mama mwenye huruma; uzima, tulizo na matumaini ya binadamu, katika Moyo wake usiokuwa na doa aangalie furaha ya binadamu wanaosafiri kuelekea mbinguni kwa Baba wa milele; anamwomba ayatazame mateso na mahangaiko ya familia ya binadamu, inayolia na kulalamika huku bondeni kwenye machozi! Analiombea Kanisa furaha inayobubujika kutoka kwenye Moyo Safi wa Bikira Maria usiokuwa na doa, ili aweze kuimarisha matumaini ya watoto wa Mungu na hatimaye, kuwaunganisha wote!

Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, Mama mpole, mwema na mpendelevu, Malkia wa Rozari Takatifu, ili kwa mfano wa Watakatifu Francis na Yacinta Marto, wale wote wanaojisadaka na kuwekwa wakfu kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili, waweze kutoka kifua mbele na kuanza hija ya mapambano dhidi ya kuta za utengano, kwa kuwaendea wale wanaoishi pembezoni mwa jamii, ili kuwashuhudia haki na amani ya Mungu; Kwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, kwa Kanisa; kuvaa mavazi meupe yaliyooshwa kwa damu azizi ya Mwanakondoo wa Mungu; damu inayoendelea kumwagika katika vita inaharibu dunia wanamoishi watu. Anamwomba awasaidie walimwengu kutambua uwepo hai na endelevu wa Mungu kati pamoja na watu wake kama ilivyokuwa jana, leo na hata milele!

Baba Mtakatifu katika sala yake anasema, Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia wa Rozari Takatifu, amebarikiwa kuliko wanawake wote, ni sura ya Kanisa iliyovishwa mwanga wa Pasaka; Yeye ni heshima ya watu wa Mungu; mshindi dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo! Bikira Maria ni shuhuda wa unabii wa upendo wa huruma ya Mungu; mwalimu mahiri wa Habari Njema ya Mwana wa Mungu, alama ya moto wa Roho Mtakatifu. Huku bondeni kwenye furaha na machozi, Bikira Maria awafundishe watoto wake ukweli wa milele ambao Baba wa milele, anapenda kuwafunulia wadogo. Awaoneshe ulinzi na tunza ya mkono wenye nguvu! Moyo wake usiokuwa na doa uwe ni kimbilio la wadhambi, njia inayowaelekeza kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na ndugu zake wote katika imani, matumaini na mapendo, wanajiaminisha kwa Bikira Maria na kujiweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu, ili kumtolea Mungu utukufu, milele yote! Amina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.