2017-05-13 16:09:00

Jifunzeni ukarimu, ushupavu na sadaka ili kuwahudumia watu wa Mungu!


Mara baada ya Baba Mtakatifu Francisko kusali na kujikabidhi mbele ya Bikira Maria wa Fatima na hatimaye, kuongoza Rozari Takatifu, Ijumaa, usiku, tarehe 12 Mei 2017, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliongoza Ibada ya Misa Takatifu iliyofurika kwa umati mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni ushuhuda wa watu wa Mungu wanaomkimbilia Bikira Maria, wakiomba awaombee mbele ya Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na dunia. Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili ni kielelezo cha ushindi dhidi ya mwovu Shetani.

Ni Mama anayejitaabisha kuwaangalia watoto wake, ili kuwafariji na kuwatangazia Injili ya matumaini na kuwahakikishia kwamba, Moyo wake usiokuwa na doa, hatimaye, utashinda. Bikira Maria anawataka waamini kuwa na imani kwani hatimaye, upendo na amani vitashinda kwa sababu huruma ya Mungu ina nguvu zaidi kuliko ubaya, kwani lile ambalo linaonekana kushindikana kwa binadamu, linawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Bikira Maria anawahimiza watoto wake kusali Rozari Takatifu, kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu; kwa kujiweka wakfu na kujiaminisha kwake ili aweze kuwaongoza. Ikiwa kama watatekeleza maagizo haya ya Bikira Maria, kwa hakika amani itaweza kutawala tena!

Kardinali Parolin katika mahubiri ametumia fursa hii kulishukuru Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kuyawezesha mamilioni ya watu kushikamana kwa ajili ya kuombea amani duniani, kiasi kwamba, Moyo Safi wa Bikira Maria umepata makazi katika nyoyo za watu kwa kuwa ni chemchemi ya matumaini na faraja; maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yakawa ni sherehe upendo; na dunia ikawekwa wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria usiokuwa na mawaa, ushuhuda unaonesha uso wa Kanisa la Kristo!

Miaka 100 imekwisha kuyoyoma tangu Bikira Maria alipowataka watu kujikita katika kuombea amani duniani! Leo hii kuna watu wanaishi katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; watu wanaishi katika hofu na wasi wasi mkuu, kiasi cha kutishiwa na hofu ya kifo, mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia; kuna changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; watu wamejikitia tamaa kwa kesho iliyo bora zaidi! Kumbe, sala bado ina nafasi ya pekee katika kukomesha vita kadiri ya mpango wa Mungu.

Bado kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mungu pamoja na kujiaminisha mbele ya Bikira Maria, ili kutangaza na kushuhudia upendo dhidi ya ubaya na dhambi. Waamini wasikubali kuzamishwa na kuendeleza ubaya, bali wawe na ujasiri wa kufanya malipizi ya dhambi za binadamu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kristo Yesu ni kielelezo cha upendo wenye huruma, uliofikia hatima yake pale juu Msalabani; akathubutu hata kuwasamehe watesi wake. Kifo chake kikawa ni fidia ya dhambi za binadamu. Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni amani na upatanisho wa watu wake! Yesu amekuwa ni ngome na kinga ya watu wake, changamoto kwa waamini ni kujiaminisha kwake katika imani na kuendelea kufuata nyayo zake na kwa kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha.

Kardinali Parolin anawataka waamini kujifunza ukarimu na ujasiri wa Bikira Maria ili kujisadaka, ili aweze kuendelea kuishi kati pamoja na watu wake; kwa kutoa mikono yao, ili Yesu aendelee kuwafariji wanyonge na maskini; miguu yao, ili Kristo aweze kuwatembelea na kuwahudumia wenye shida; watolee mabega yao, ili kuwainua na kuwategemeza wanyonge pamoja na kuendelea kutekeleza kazi katika shamba la Bwana; akili zao zijielekeze daima katika kutekeleza mapenzi ya Mungu. Hivi ndivyo walivyojitahidi kufanya Watakatifu Francis na Yacinta Marto pamoja na Mtumishi wa Mungu Lucia dos Santos. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima iwe ni fursa ya kumwimbia Bikira Maria utenzi wa “Magnificat”, kwa sababu ameuangalia unyonge wa mjakazi wake na huruma yake hudumu kizazi baada ya kizazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.