2017-05-12 18:12:00

Mmevikwa utu mpya katika Kristo Yesu!


Ndugu msikilizaji, Mzaburi anatualika kiasema: “Mwimbieni Bwana Wimbo Mpya kwa maana ametenda mambo ya ajabu, machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.” Fumbo la Pasaka linaufanya upya ubinadamu wetu. Mwanadamu anafanyika upya katika Kristo kwa kushirikishwa umungu kwani anafanyika kuwa mwana mrithi. Hii ndiyo sababu mzaburi ameianza Dominika hii kwa kututaka kudhihirisha upya huo wa maisha: “Mwimbieni Bwana Wimbo mpya!”. Ndiyo ni haki kuuimba wimbo huu daima kwani ametenda maajabu katika maisha yetu. Ni wimbo mpya wala si wimbo wa kale; ni maisha mapya na si yale ya zamani. Katika sala ya mwanzo ya Liturujia ya Dominika hii tumedhihirisha kuufahamu upya huu na hivyo tumemwomba Mungu tukisema: “tunakuomba utusikilize kwa wema sisi wanao, ili katika kumwamini Kristo tupate uhuru wa kweli na urithi wa milele”.

Ni katika upya huu wa maisha na uhuru wa kweli ndipo tunaweza kuuelewa muktadha wa Injili ya leo ambayo inaanza kwa kutuambia: “Msifadhaike mioyoni mwenu”. Mwana huru hana sababu ya kufadhaika kwa sababu hakuna kinachomfunga na kumyima uhuru. Mtumwa ndiye yule anayekuwa katika hali ya wasiwasi. Akiamka asubuhi hana uhakika na kitakachotokea mbele yake; daima yupo katika taharuki kuisikiliza amri ya Bwana wake. Ila sisi tumekombolewa na tumefanywa kuwa wana huru. Tunaijua njia ya kupitia, tumelekezwa ukweli na tumeshirikishwa uzima wa kimungu. Tunaipokea hadhi hiyo kwa njia ya Kristo ambaye anajitambulisha kwetu kuwa ni “njia, ukweli na uzima”. Kristo ni sababu ya matumaini kwetu. Ufufuko wake ni ushindi na sababu ya matumaini kwetu. Ufufuko wa Kristo ni uthibitisho kwetu wa kuwa wana huru wa Mungu na hakika ya kurithi ufalme wa Mungu.

Kristo anathibitisha kuwa kweli ni Njia kwa sababu alituonesha njia ya kufika kwa Baba na kuwa wana wake. Njia hiyo ni utii na unyenyekevu: “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyeyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu (Mt 11:29). Utume wake wake wote ulituonesha njia hiyo. Hakutumia mabavu, hakuwadharau wengine na wala hakujikinai katika kuweza yote. Daima alitafuta mapenzi ya Mungu na kuyatimiza. Njia hii ndiyo ilimfikisha katika fumbo la Pasaka na kwa ushindi wake anatupatia kielelezo cha kufuata kwa ajili ya kuwa wapya kimaisha na wana huru wa Mungu. Dini ya kweli inatupeleka katika mahusiano sahihi kati yetu na Mungu. Yeye ametufunza namna ya kuhusiana na Mungu kama watoto wake, yaani katika hali ya unyenyekevu. Hili hujifunua vizuri katika sala ambapo tunainua miyo yetu kwa Mungu na kujiweka chini yake kama watoto wake.

Kwa ufufuko wake Kristo anathibitisha kuwa kweli ni ukweli kwani ametufundisha dini ya kweli. Ukweli huu unapigilia msumari uhakika wa njia aliyotuonesha. Pengine hatujiulizi ukweli ni upi au twajifanya hatuujui ukweli. Ukweli huu hujifunua kwetu kwa mafunuo mbalimbali na mafundisho ndani ya Kanisa. Njia pekee ya kuuona ukweli huu ni kuupokea kama Neno na mwanga si kujibu matakwa yetu na hamu zetu bali kuwa kielelezo cha maisha yetu na ukristo bora. Wengi tunakosa fadhila ya unyenyekevu na pengine kuipoteza nafasi hii adimu kwa sababu ya kiburi chetu cha kibinadamu na kujikinai kuwa na uwezo wa kufikiri na kufanya tafiti nyingi za kisayansi na kijamii. Katika kiburi chetu hiki hatuioni nafasi ya Mungu na wakati mwingine hupumbazwa na matokoe chanya ya tafiti zetu hizi. Matokeo yake ni kuendelea kubaki katika ukale wa maisha na kutompatia Mwenyezi Mungu nafasi inayomstahili.

Kwa ufufuko wake Kristo anathibitisha kuwa ni uzima kwa kutushirikisha uzima wa kimungu na kutufanya wana warithi wa Mungu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kwamba “kwa njia ya Ubatizo tunafanywa huru toka dhambi na tunazaliwa upya kama watoto wa Mungu, tunakuwa viungo vya Kristo na tunaingizwa katika Kanisa na tunafanywa washiriki wa utume wake.” (KKK 1213). Sakramenti ya Ubatizo ndiyo inatushirikisha fumbo la Pasaka la Kristo kwani “tulizikwa pamoja naye kwa njia ya Ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo nasi tuenende katika upya wa uzima” (Rum 6:4). Huku ndiko kuzaliwa mara ya pili au kuzaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu ambako Kristo alimwambia Nikodemu kama njia pekee ya kuurithi ufalme wa mbinguni (Rej Yoh 3:1 – 7).

Maisha ya ukristo ni upya wa maisha. Upya huu wa maisha ndiyo sababu ya nguvu na matumaini katika maisha yetu. Upya huu wa maisha huthibitisha uwepo wa Kristo ambao huonekana katika kazi zake. Kristo ni uthibitisho au uhakika wa uwepo wa Baba kati yetu. Kazi zake ni uthibitisho huo na kazi kubwa na kilele cha yote ni Fumbo la Pasaka, muujiza mkubwa ambao unafumbatwa katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu sana. Maisha ya Mkristo yanayopambwa na uwepo wa Mungu hugeuka kuwa sababu ya nguvu na matumaini si kwake tu bali kwa watu wote. Haya ni maisha ambayo yanapambwa na fadhila za kikristo ambazo zinafumbatwa katika lengo moja tu la ukombozi wa mwanadamu. Mkristo anapoithibitisha vema haiba yake ya kikristo ni sababu ya upendo kwenye chuki, umoja katika utengano, heshima katika dharau na yote haya humpeleka katika dini safi na ya kweli yaani kumpatia mwanadamu nafuu katika maisha!

Maisha ya Mkristo si sawa kama na Wayahudi ambao kwao Kristo amekuwa kama “Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha”. Hawa ni wale wanaotumia mbinu na hila zote kumwondoa Kristo Mfufuka katika maisha ya mwanadamu. Hapa ni kuyaweka mbele yetu matendo yote ya upinzani dhidi ya mafundisho ya imani yanayotolewa na Kanisa. Kristo ameweka katika Kanisa utume wa kufundisha ukweli wote: “Enendeni ulimwenguni kote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa” (Mk 16:15 – 16). Upinzani huu dhidi ya ukweli wa kiinjili kwa hakika huleta hofu na mashaka katika maisha ya mwanadamu. Pale dunia inapofumbia macho Neno la Mungu na kumsogeza Kristo pembeni chuki hutawala, unyonyaji ustawi na machafuko huwa ni hadithi ya kila siku. Mtume Petro anatuhasa akisema: “Mwendeeni yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai mmejengwa muwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zitakazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo”.

Katika hali hii ya kuwa wana wa Mungu katika Kristo tunapokea utume wa kudumisha umoja na kila mmoja kufanya nafasi yake kwa manufaa ya jamii yote ya waamini. Mgawanyo wa majukumu katika jamii huleta afya katika mahusiano, hutoa fursa ya kushirikishana vipaji, hutufunulia umuhimu wa kutegemezana katika maisha na huongeza na kuthamini heshima na mchango wa kila mtu katika jamii. Kujilimbikizia na kujikinai kuweza vyote hujenga chuki na mdororo wa kijamii. Hili halipaswi kuonekana katika jamii ya waliozaliwa upya katika Kristo. Tujenge umoja huo kwani sote tunacho kielelezo kimoja ambacho ni Kristo aliye Njia, Ukweli na Uzima.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.