2017-05-11 11:18:00

Mifumo yote ya utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!


Baba Mtakatifu Francisko tangu aingie madarakani miaka minne iliyopita, amesimama kidete kwa maneno na matendo kupinga vitendo vyote vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hakusita kusema wazi wazi kwa macho makavu kwamba: biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu; ni kashfa kubwa katika ulimwengu mamboleo na ni uvunjaji wa haki msingi za binadamu unaojionesha katika kiwango cha kimataifa kiasi hata cha kugusa sekta ya utalii duniani.

Haya yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa alipokuwa anachangia hoja kuhusu mjadala wa biashara haramu ya binadamu katika maeneo yenye vita, kazi za suluba, utumwa mamboleo pamoja na mifumo yake. Amewaambia wajumbe wa Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, chanzo kikuu kinachopelekea mafuriko ya biashara haramu ya binadamu pamoja na mifumo ya utumwa mamboleo ni umaskini wa hali na kipato; ni dalili za kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Watu wanaotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo ni wale wanaokabiliwa pamoja na mambo mengine na ujinga, fursa za ajira au majanga asilia.

Ni watu wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, lakini kwa bahati mbaya wanajikuta wakiwa wametumbukizwa katika vitendo vya unyanyasaji na dhuluma kiasi cha kuweka utu na heshima yao rehani. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inaendelea kuzalisha mamilioni ya wakimbizi na wahamiaji wanaotengenezewa mazingira rahisi sana ya kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, kiasi kwamba, biashara hii kwa sasa iko katika kiwango cha kitaifa na kimataifa, kama hali inavyojionesha huko Mashariki ya Kati.

Ukosefu wa jitihada za makusudi za kupambana na hatimaye, kuwafikisha wahusika kwenye mkondo wa sheria, kumepelekea biashara hii haramu kuendelea kushamiri miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa licha ya matamko mbali mbali yanayotolewa na viongozi wa kitaifa na kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kinachokosekana hapa ni utashi wa kisiasa na uwajibikaji wa kimaadili kwani biashara haramu ya binadamu ni uvunjaji wa haki msingi za binadamu na sheria ya kiutu kimataifa. Wahanga wa biashara hii wanapaswa kuokolewa, kulindwa pamoja na kuhakikisha kwamba, sheria inachukua mkondo wake.

Askofu mkuu Bernardito Auza anasema, Ujumbe wa Vatican unalaani kwa nguvu zote biashara haramu ya silaha ambayo imepelekea silaha za hatari kuangukia kwenye makundi makubwa ya kigaidi, kiasi cha kuendelea kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo, mauaji, nyanyaso na dhulumua dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Biashara ya magendo ya silaha, utumwa mamboleo na mifumo yake yote ni mambo yanayoendelea kushamiri kila kukicha kwenye ngazi ya kitaifa na kimataifa. Vatican inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti biashara ya silaha kwa kuzingatia itifaki za kimataifa, ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Utawala wa sheria unaofumbatwa na utashi wa kisiasa na uwajibikaji wa kimaadili ni nyenzo msingi katika kupambana na biashara haramu ya silaha, binadamu, utumwa mamboleo pamoja na mifumo yake yote. Wahusika washughulikiwe kikamilifu kisheria, ili kweli haki iweze kutendeka.

Baba Mtakatifu Francisko anaichangamotisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatekeleza kwa vitendo itifaki na makubaliano mbali mbali dhidi ya biashara haramu ya binadamu, silaha na mifumo yote ya utumwa mamboleo, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Jambo la msingi ni kuendeleza kampeni ya uragibishaji wa uwepo na madhara ya biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake yote. Serikali, vyombo vya sheria, wafanyakazi pamoja na wadau mbali mbali wanapaswa kushirikiana ili kuokoa maisha, utu na heshima ya wanawake, wasichana na watoto wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo. Ni dhamana na jukumu ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mstari wa mbele ili kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unatekelezwa na kudumishwa na wote, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, ili kweli haki na amani viweze kushamiri kati ya watu wa mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.