2017-05-09 14:19:00

Papa: Pokeeni Neno la Mungu kwa unyenyekevu ili liwapatie amani!


Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, ili waweze kulipokea na kulimwilisha Neno la Mungu, ili liweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao. Mwamini akijikita katika Neno la Mungu linakuwa kwake chemchemi imnayobubujikia: wema, amani pamoja na kujiamini. Kumbe, waamini wanapaswa kulipokea, kulifahamu na kuwa na mazoea ya Neno la Mungu. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 9 Mei 2017 katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea pia Watawa wanaohudumia Hosteli ya Mtakatifu Martha, Kanisa linapomkumbuka Mtakatifu Luisa wa Marillac.

Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, katika tafakari zake zilizopita aligusia jinsi ambavyo waamini wanaweza kuwa na shingo ngumu kiasi cha kushindana na Roho Mtakatifu kama walivyofanya wakuu wa Makuhani na waandishi. Liturujia ya Neno la Mungu, inaonesha ile hamu na tabia ya unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu inayopaswa kuoneshwa na Wakristo. Baada ya adha kuu ya Kanisa lililokuwa katika Yerusalemu, wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria isipokuwa Mitume ndio waliobaki mjini Yerusalemu. Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki walisafiri na kwenda hadi Kipro, Foinike, Antiokia na Kirene. Baadhi ya watu wakaonesha unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu na kuanza kusikiliza Neno la Mungu.

Mtume Yakobo katika Waraka wake wa kwanza kwa watu wote anawaalika waamini kulipokea Neno la Mungu kwa unyenyekevu, bila kufanya shingo ngumu, bali wazi na wanyofu. Neno la Mungu linapaswa kupokelewa katika moyo mnyofu, ili kulifahamu na kwa kulifahamu Neno la Mungu, mwamini anapata nafasi ya kumfahamu Kristo Yesu, ambaye watakuwa tayari kuisikiliza sauti yake na kumfuasa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga mazoea matakatifu na Neno la Mungu, kwa kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Kwa njia hii, Neno la Mungu linakuwa ni chemchemi wema, furaha, amani, upole, huruma na hali ya kujiamini.

Huu ndio mtindo wa maisha unaojinyenyekesha mbele ya Roho Mtakatifu, ili kulipokea Neno la Mungu na kulimwilisha ili liweze kuzaa matunda ya: huruma, wema, amani na mapendo, tunu msingi katika maisha ya Kikristo! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mitume waliposikia kwamba, Habari Njema ya Wokovu ilikuwa inazidi kuenea kwa kasi, walishikwa na hofu kidogo, lakini mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, kiasi kwamba watu wengi wakaamini na kumwongokea Mungu. Wanafunzi wa Antiokia wakawa wa kwanza kuitwa Wakristo! Mtume Barnaba alitumwa kushuhudia hayo yaliyokuwa yanasemwa, alipoiona neema ya Mungu, akafurahi na kuwataka wote kuambatana na Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kwani walikuwa kweli ni watu wema waliojaa Roho Mtakatifu na imani. Hii ni changamoto kwa waamini kumpokea Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza njia na kuwafundisha Neno la Mungu, tayari kulimwilisha katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.