2017-05-06 15:33:00

Siku ya 54 ya Kuombea Miito Duniani: Masista wa Mama Yetu wa Usambara!


Tangu mwanzo wa Kanisa, kumekuwepo na watu waliojisadaka na kujitoa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; kwa kuishi mashauri ya Kiinjili yaani: Usafi kamili kwa ajili ya Ufalme wa Mungu na upendo kwa wote, ili kusaidia kueneza wema, maisha ya uzima wa milele na sadaka kwa wote! Ufukara huwawezesha watawa kushiriki ufukara wa Kristo Yesu aliyekuwa tajiri, lakini akajishusha na kuwa fukara ili sisi tuwe matajiri kwa ufukara wake. Hii ni changamoto ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini ambao ni walengwa na amana ya Kanisa. Watawa kwa kuweka nadhiri ya utii, wanamtolea Mungu kabisa utashi wao kama sadaka ya nafsi zao, na kwa njia ya sadaka hiyo wanajiunga na mapenzi ya Mungu yanayopania kuokoa, kwa namna ya kudumu na halisi. Kwa njia ya utii watawa wanajifunga zaidi na utumishi wa Kanisa, kwa kujitahidi kumfuasa Kristo zaidi!

Shirika la Masista wa Mama yetu wa Usambara lilianzishwa kunako mwaka 1954 na Askofu Eugene Arthurs wa Jimbo Katoliki Tanga, akisaidiwa na Wamisionari wenzake wa Shirika la Mapendo, maarufu kama Warosiminiani, huko Rangwi, Wilayani Lushoto, Tanga. Lengo la kuanzisha Shirika la Masista wa Mama Yetu wa Usambara lilikuwa ni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya mashauri ya Kiinjili, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu, Ibada kwa Bikira Maria na huduma makini kwa familia ya Mungu.

Watawa wanapotekeleza yote haya kwa ari na moyo mkuu, wanashiriki pia katika mchakato wa kupyaisha maisha yao na kuendelea kuchuchumilia utakatifu wao binafsi unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika maisha ya pamoja kama wanajumuiya! Karama ya Shirika la Masista wa Mama Yetu wa Usambara ni uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Tunatambua kwamba, sisi ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma, mapendo na matumaini kwa watu wa Mungu, ndiyo maana roho ya shirika inajikita katika upendo kwa Mungu na jirani!

Shirika letu linaendelea kujisadaka katika kufundisha dini kwa watu wa marika mbali mbali kwa kukazia katekesi makini ambayo kimsingi ni muhtasari wa: imani ya Kanisa, Sakramenti za Kanisa ambazo ni chemchemi ya neema, baraka na maisha ya uzima wa milele; Amri za Mungu ambazo ni dira na mwongozo wa maisha  katika uadilifu na utu wema. Katekesi ni muhtasari wa maisha ya sala yanayojenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu. Masista wetu, wameendelea kushiriki utume wa Kristo mganga mkuu wa maisha ya kiroho na kimwili kwa kutoa huduma makini kwa wagonjwa, lakini kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa wanatufunulia Uso wa Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake! 

Tunatambua kwamba, ili kujenga nchi bora, tunahitaji kuboresha elimu na ukitaka kuwa na elimu bora na makini huna budi kuboresha hali ya walimu na kama kweli unataka taifa linaloheshimika mbele ya mataifa lazima uheshimu walimu! Watawa wetu wamejikita katika huduma ya elimu bora ili kuwajengea vijana wa kizazi kipya imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora. Watawa wetu wanaendelea kujisadaka pia katika mchakato wa maendeleo endelevu ili kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi.

Masista wa Mama Yetu wa Usambara wanatekeleza utume wao Jimbo Katoliki la Tanga, Moshi pamoja na Jimbo kuu la Dar es Salaam. Tunafanya utume wetu pia nchini Kenya na Italia. Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wasichana wanaojisikia kuwa na wito wa maisha ya kitawa, wasisite kumfungulia Mungu malango ya matumaini yao. Wawashirikishe Mapadre wao, wataweza kuwasaidia zaidi, ili kweli waweze kutekeza mpango wa Mungu katika maisha na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

 

Na Sr. Salome Robert Sheshe.

Shirika la Masista wa Mama Yetu wa Usambara.








All the contents on this site are copyrighted ©.