2017-05-05 15:14:00

Changamoto za mawasiliano: teknolojia na majiundo ya wafanyakazi!


Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican vinapaswa kujikita zaidi na zaidi katika kutangaza upendo na huruma ya Mungu kwa walimwengu, kwa kuzingatia: utume wa Mama Kanisa na dhamana ya Kimissionari. Kipaumbele kitolewe hususan kwa maskini, waliotengwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yanawezesha watu kupata ujumbe kwa njia ya maandishi, sauti na picha kwa wakati mmoja.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 4 Mei 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican. Anasema, hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanaendeleza mchakato wa mageuzi kwa vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kwa kusoma alama za nyakati yaani: kwa kuzingatia: uzalishaji na ugavi wa huduma ya mawasiliano ya jamii kwa kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini vigenzo na nyenzo zitakazosaidia kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu kwa watu wote.

Kwa upande wake, Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican anasema, kuna ushuhuda unaonesha kwamba, tema ya mawasiliano ndani ya Kanisa na kwa ajili ya Kanisa ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko anayepania kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu ili kusakafia umoja na udugu; upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Wanahabari Wakristo wanayo changamoto kubwa sana mbele yao yaani: kutambua, kusikia na kuonja wema wa upendo wa Mungu kwa waja wake, kwa njia ya waamini kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu. Kwa njia hii, wanabahatika kupata nyenzo na vigezo msingi vinavyoweza kutumika kwa ajili ya kuboresha, kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili vinginevyo, maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari hayatakuwa yamesaidia kitu!

Monsinyo Dario Edoardo Viganò akaza kusema, changamoto ya pili ni kuhakikisha kwamba ili kuweza kusoma alama za nyakati sanjari na kwenda na kasi kubwa ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya habari, kuna haja kwa Kanisa kujikita katika majiundo makini na endelevu yatakayowapatia wahudumu wa vyombo vya habari vya Kanisa weledi, ujuzi, maarifa na teknolojia ili kweli Injili ya huruma ya Mungu iweze kuwafikia watu wengi zaidi. Changamoto hizi bado zinaendelea kufanyiwa kazi na Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.