2017-05-02 10:48:00

Papa Francisko: Sera na mikakati ya uchumi ijikite katika udugu!


Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 2 Mei 2017 imekuwa ikifanya mkutano wake wa mwaka, ambao umeongozwa na kauli mbiu “Kuelekea kwenye Jamii shirikishi, njia mpya za mkamilishano”. Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya wajumbe wote amemtumia ujumbe maalum Professa Margaret Archer, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii akikazia kwa namna ya pekee: udugu kama kanuni msingi wa sera na mikakati ya kiuchumi. Amewaalika wajumbe kupembua kwa kina na mapana zaidi dhana ya haki; maendeleo endelevu ya binadamu; umuhimu wa kazi kama utimilifu wa utu na heshima ya binadamu na changamoto kwa watu kuondokana na ubinafsi!

Baba Mtakatifu anapenda kuwapongeza wajumbe kwa kuchagua mada ya ushirikishwaji wa jamii kadiri ya dhamana, wajibu na weledi wao katika masuala haya, ili kweli watu wengi zaidi waweze kushirikishwa katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali inayogusa maisha yao kwa kutambua kwamba, jamii ni wadau wakuu wa maendeleo endelevu. Ushirikishwaji huu unapaswa kuzingatia: mafao ya wengi, sheria, kanuni na taratibu kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa utekelezaji wa haki pamoja na kusimama kidete kuendeleza mafao ya wengi kwa wale wote wanaoshiriki.

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kupanua zaidi dhana ya haki kadiri ya Mapokeo kwa kuanzia katika mchakato wa uzalishaji na ugawanaji wa faida iliyopatikana. Katika masuala ya uzalishaji na huduma; wafanyakazi wanapaswa kupewa mshahara unaokidhi mahitaji yao msingi sanjari na kuzingatia: utu, heshima na haki zao msingi mintarafu kanuni maadili na utu mwema. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikazia kwa namna ya pekee  kanuni na taratibu katika maisha ya kiuchumi na kijamii katika ujumla wake. Mfumo wa kazi hauna budi kuzingatia madai ya binadamu, maisha yake, dhamana na majukumu yake katika familia. Wafanyakazi wanawajibika kutumia muda, bidii na weledi katika mchakato mzima wa uzalishaji na utoaji huduma.

Wafanyakazi wapewe muda wa kupumzika na kushughulikia: ukuaji na ustawi wa familia zao. Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa namna ya pekee yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa udugu kama kanuni msingi na kiini cha sera na mikakati ya kiuchumi. Udugu unakamilishwa na mshikamano badala ya kuzingatia  tu tija katika mchakato mzima wa uzalishaji. Udugu kiwe ni kipimo cha mahusiano na mafungamano ya kijami. Udugu ni dhana inayofumbatwa katika Maandiko Matakatifu kwa kukazia anasema Baba Mtakatifu mshikamano wa dhati unaotambua na kuthamini uwepo wa jirani, utu na heshima yao; uhuru na haki zao msingi pamoja na ushiriki wao katika mchakato mzima wa mafao ya wengi kadiri ya nafasi, uwezo, wito, mpango wa maisha na karama katika huduma.

Udugu ni mwendelezo wa Fumbo la Umwilisho katika maisha ya mwanadamu na watu watahukumiwa kadiri wanavyowatendea jirani zao. Katika historia ya binadamu kwa karne za hivi karibuni kumekuwepo na vita ya kisiasa na kitamaduni, iliyotaka kusimamia mshikamano na haki na huo ukawa ni mwanzo wa vyama vya wafanyakazi vilivyodai haki msingi za kijami na kisheria; mapambano ambayo kwa bahati mbaya bado hayajafikia kileleni mwake. Baba Mtakatifu anasema, hii inatokana na ukweli kwamba, kuna umati mkubwa wa watu unaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii; hakuna ugawanaji wa utajiri na rasilimali ya dunia katika hali ya usawa; kumekuwepo na soko huria kwa wenye nguvu kuwanyanyasa wadogo na wanyonge; utu na heshima ya binadamu bado haujafikiwa kwa kiwango cha kuridhisha; uhuru, ufahamu, utambulisho, haki na mkamilishano ni mambo ambayo bado yanaelea kwenye ombwe na waathirika wakuu ni wananchi wa kawaida. Matokeo yake ni migogoro, kinzani na mipasuko ya kijami kutokana na watu wachache kuendelea kufaidika na rasilimali pamoja na utajiri wa dunia.

Watu wengi wanaendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini, vita, athari za mabadiliko ya tabianchi zinazowaathiri watu zaidi ya milioni 65 wanaolazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kuna mamilioni ya watu, wametumbukizwa katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, kiasi kwamba, leo binadamu amegeuka kuwa kama bidhaa sokoni, anaweza kupigwa mnada! Ukoloni mamboleo katika masuala ya kiuchumi, umepelekea kuibuka kwa makundi ya kijamii, kwa watu wachache kuwa na utajiri wa kutisha na mamilioni ya watu kuendelea kuishi kwa taabu sana. Huu ndio uchumi wa fedha, sabuni ya roho!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hizi ni Sera na mikakati inayopaswa kubadilishwa ili kujenga na kuimarisha uchumi shirikishi unaofumbatwa katika udugu na mshikamano wa dhati, ili hatimaye, kuondokana na ukosefu wa usawa kijami unaofumbatwa kwa namna ya pekee na ubinafsi, uchoyo na hali ya kumezwa mno na malimwengu. Kuna haja ya kudhibiti mfumo wa fedha badala ya kushughulikia athari zake katika maisha ya watu! Papa Francisko anasema, anapenda pia kukazia umuhimu wa maendeleo endelevu ya binadamu yanayofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu; uhuru katika maana yake pana zaidi, yaani uwezo wa kupanga na kuchagua mambo msingi katika maisha; wito na mafao ya wengi. Uhuru ni chanda na pete na uwajibikaji unaowataka watu kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anasema, katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya jamii, kazi inapaswa kufahamika kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu na utimilifu wa maisha na utu wa binadamu. Kazi inamshirikisha mwanadamu katika kazi ya uumbaji, ili kutengeneza dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya wa maana ya kazi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mfanyakazi mwenyewe na kamwe asigeuzwe kuwa ni mtumwa wa kazi au kwamba, anaweza kufukuzwa kazi wakati wowote na nafasi yake kuchukuliwa na mashine. Kumbe, hapa kuna haja ya kuzingatia haki ya kazi, kwa kupata mshahara unaotosha mahitaji msingi na utu wake kama binadamu. Sehemu ya kazi ni mahali pa majiundo makini panapomfunda mfanyakazi kumwilisha tunu msingi za maisha ya kazi na huduma.

Taasisi za elimu viwe ni vituo vya: elimu, weledi, ujuzi na mafunzo yatakayowawezesha wanafunzi wanapohitimu masomo yao kuishi vizuri, kwa kuwajibika, daima wakitafuta mafao ya wengine badala ya kujikita katika ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko! Uhuru ukuze na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii kwa kumhusisha pia Mwenyezi Mungu. Karne ya ishirini na moja inakabiliwa na changamoto nyingi za: kijami, vita, utumwa mamboleo, athari za mabadiliko ya tabianchi; wakimbizi na wahamiaji; haki ya utu wa mtu kisiasa na haki ya utu wa mtu. Hizi ni changamoto mpya zinazopaswa kuangaliwa kwa upana mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafuta kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote watapewa kwa ziada. Watu wajizatiti zaidi kukuza na kudumisha: udugu, uhuru, haki, amani na utu wa binadamu wote, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya neema, ili kueneza huruma ya Mungu, hatimaye, kujenga udugu na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.