2017-05-01 13:13:00

Mwenyeheri Leopaldina Naudet!


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Ijumaa, tarehe 28 Aprili 2017 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Leopaldina Naudet, kuwa Mwenyeheri huko Jimboni Verona, Italia. Mwenyeheri Leopaldina Naudet alizaliwa kunako tarehe 31 Mei 1773 huko Firenze. Akabahatika maisha yake kuishi huko Italia, Ufaransa na Vienna, Austria.

Kardinali Angelo Amato anasema, utakatifu si vazi ambalo mwamini anaweza kujitwalia sokoni, bali ni neema anayojaliwa na Roho Mtakatifu, kiasi kwamba, anaweza kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo na hivyo kuwa mfano bora wa kuigwa na waamini wengine katika hija ya maisha yao, daima wakijitahidi kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Mwenyeheri Leopaldina Naudet katika maisha yake, alimwona Bikira Maria kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake ya kiroho, kiasi cha kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu akisema, mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena!

Hiki kikawa ni kisima na chemchemi ya utakatifu wa maisha yake, akaonja na kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika safari yake ya maisha hapa duniani. Akakuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa; akaendelea kujibidisha katika utu wema na adabu njema, kiasi cha kuwa ni kivutio kikuu kwa jirani zake. Yote haya aliyafanya kwa moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa, kiasi hata cha kumwezesha kutekeleza dhamana na majukumu yake huko Vienna na Prague. Mwenyeheri Leopaldina Naudet alibahatika kuwa na neema na baraka nyingi zilizomwandama katika maisha yake.

Kunako mwaka 1809 akaanzisha Shirika la Watawa wa familia Takatifu na kuwa Mama mkuu wake wa kwanza. Akawa kiongozi ambaye alitumia muda wake mwingi kwa ajili ya kuabudu Ekaristi Takatifu; akajiaminisha kwa Mungu katika huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Akawa kweli ni shuhuda wa imani iliyokuwa inamwilishwa katika matendo. Akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa maskini kupata elimu bure! Akawasaidia watu kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho kwa njia ya mafungo makini, huku akiwahimiza watawa wake kuhakikisha kwamba wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika Injili ya upendo.

Mwenyeheri Leopaldina Naudet akayapamba maisha na utume wake kwa harufu nzuri ya utakatifu wa maisha, akawa ni mfano bora wa kuigwa kama mfuasi amini wa Kristo Yesu na shuhuda wa upendo wa Mungu unaojionesha kwa njia ya Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Yesu akawa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha, huduma na majitoleo yao kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mfano bora wa kuigwa katika imani na matumaini, kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu ambaye alimfufua Mwanaye wa pekee kutoka kwa wafu akampatia utukufu, hata imani na matumaini yao yanabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kardinali Angelo Amato anasema, matumaini yanawahimiza waamini kujichimbia katika utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.