2017-04-30 12:58:00

Salam na matashi mema kutoka kwa Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hija yake ya kumi na nane ya kimataifa huko Misri na kurejea tena mjini Vatican, Jumamosi usiku, tarehe 29 Aprili 2017. Itakumbukwa kwamba, hija hii imeongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri”. Amekazia umuhimu wa kuondokana na vita pamoja na mashambulizi ya kigaidi kwa misingi ya kidini, jambo ambalo ni kufuru kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha uekumene wa sala na maisha ya kiroho; uekumene wa damu na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Majadiliano ya kidini yasaidie kukuza na kudumisha uwajibikaji wa pamoja kwa kwa kusimama kidete: kulinda na kudumisha utakatifu wa maisha ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; uhuru wa kuabudu, uhuru wa dhamiri pamoja na uhuru wa kidini; ili kweli haki, amani na  maridhiano yaweze kutawala kati ya watu wa Mataifa!

Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka nchini Misri, akiwa kwenye anga la Misri, amemtumia salam na matashi mema Rais Abdel Fattah Al Sisi wa Misri pamoja na kumshukuru kwa wema na ukarimu aliounja kutoka kwa familia ya Mungu nchini Misri. Amemhakikishia sala na sadaka yake pamoja na kuwapatia wananchi wote wa Misri baraka zake za kitume, kwa kuwaombea amani na furaha.

Baba Mtakatifu alipofika kwenye anga la Ugiriki, alimtumia salam na matashi mema Rais Prokopis Pavlopoulos wa Ugiriki kwa kumwelezea kwamba, amehitimisha hija yake ya kitume nchini Misri na kwamba, anamhakikishia Rais na wananchi wake wote sala na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Kama kawaida, “alipotinga mguu” kwenye anga za Italia amemtumia salam na matashi mema, Rais Sergio Mattarella wa Italia akionesha furaha inayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake baada ya kukutana na familia ya Mungu nchini Misri wakati wa hija yake ya kitume. Anasema, Wamisri ni watu ambao wana  utajiri mkubwa wa kihistoria, kitamaduni na maisha ya kiroho. Amemtakia Rais Mattarella na wananchi wake wote, heri na baraka tele; ustawi na maendeleo na hatimaye, kuwapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.