2017-04-30 12:28:00

Papa Francisko achambua vishawishi vya mapadre na watawa!


Wakleri, watawa na majandokasisi wanapaswa katika maisha yao kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa Kristo Mfufuka, daima wakishirikiana na Wakristo  wa Makanisa mengine ili kujenga Ufalme wa Mungu nchini Misri. Kamwe wasikatishwe tamaa na matatizo pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Kanisa. Hakuna mwamini anayeweza kukwepa Msalaba unaotukuzwa na Mama Kanisa, kwani hiki ni kielelezo cha Ukombozi wa mwanadamu na ushindi wa Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Hata kama Wakatoliki bado ni wachache nchini Misri ikilinganishwa na waamini wa Makanisa na dini nyingine, hakuna sababu ya kuwa na woga wala wasi wasi, kwani hivi ndivyo inavyompendeza Mwenyezi Mungu!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi alasiri, tarehe 29 Aprili 2017 alipokutana na kusali pamoja na wakleri, watawa na majandokasisi kutoka Misri, waliokutanika kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Leo Mkuu iliyoko kwenye Makao Makuu ya Patriaki wa Kanisa Katoliki la Kikoptik, Cairo, nchini Misri. Baba Mtakatifu amewahimiza wote hawa kuamini, kushuhudia ukweli na kupandikiza mbegu ya matumaini kwa familia ya Mungu bila ya kuwa na wasi wasi wa kutaka kuvuna mapema, kwani kuna watu waliojisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, leo hii, familia ya Mungu inafaidi matunda ya jasho lao!

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kutoa angalisho makini kwa wakleri, watawa na majandokasisi kuwa makini na kamwe wasikatishwe tamaa na mambo yanayokwenda kinyume na mpango wa Mungu katika maisha. Wao wakaze uso kama gumegume kwa kutambua kwamba, wao ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia; ni vyombo vya matumaini, wajenzi wa amani na madaraja ya watu kukutana; wao ni vyombo vya majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha: haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Baba Mtakatifu amewakumbusha vishawishi wanavyoweza kukutana navyo katika maisha na utume wao kwa Mungu na jirani! Haya si mambo mageni katika maisha yao kwani tayari yalikwisha andikwa na Wamonaki kutoka Misri! Amewaka kuondokana na kishawishi cha kutaka kuwaburuza waamini katika uongozi wao, bali wawe ni mfano wa viongozi bora kwa kujikita katika kipaji cha ugunduzi katika shughuli na mikakati ya kichungaji; wawe ni faraja kwa wale wanaoteseka na kutenda wema pasi na kungoja shukrani. Wawe ni waaminifu kwa Mungu, Kristo na Kanisa lake kwani Baba yao wa mbinguni aliyeko sirini atawalipa kwa wakati wake!

Baba Mtakatifu anawataka watumishi wa Kanisa kuondokana na tabia ya litania ya manung’uniko yasiyokuwa na tija wala mvuto; kwa kuangalia daima makosa na mapungufu ya viongozi wao, bali kwao kila kikwazo kilichoko mbele yao, kiwe ni fursa ya kusonga mbele katika utekelezaji wa majukumu yao. Watu wanaopenda kulalama daima, hao ni wavivu hawataki kufanya kazi. Kishawishi kingine ni majungu, fitina na kijicho; mambo yanayowafanya wakleri na watawa kushindwa kuwa na furaha, amani na utulivu wa ndani! Ni watu ambao ni kikwazo kikubwa  cha ukuaji na ukomavu katika maisha; chanzo cha kinzani na migongano ya kijumuiya. Viongozi wa Kanisa wakumbuke daima kwamba, ni kwa njia ya wivu na kijicho cha shetani, kifo na mauti, vimeingia duniani. Wakleri na watawa watambua uwezo, karama na mapungufu yao na kamwe wasijilinganishe na wengine, kwani wanaweza kujikuta wakimezwa na kiburi pamoja na majivuno,  kaburi la utu wa binadamu!

Viongozi wa Kanisa wanapaswa kutambua kwamba, kuna tofauti ya karama na mapaji, jambo la msingi ni kusikilizana kwa dhati katika hali ya unyenyekevu na kuheshimiana ili yote haya yawe ni kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Kwa vile mambo haya anayazungumza akiwa nchini Misri, amewataka viongozi wa Kanisa wasiwe na mioyo migumu kama Farao, kwa kujikwezwa mbele ya wengine; kwa kutaka kuhudumiwa badala ya kuhudumia kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma ya unyenyekevu na yule anayetaka kuwa mkuu wa wote basi awe ni mtumishi wa wote!

Ubinafsi, uchoyo na ”mkono wa birika” ni kishawishi kingine ambacho viongozi wa Kanisa wanapaswa kukikwepa kwa kudhani kwamba bila wao, mambo hayaendi! Lakini, Kanisa ni Jumuiya ya waamini, ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo na kwamba, wokovu wa mtu mmoja unafumbatwa katika utakatifu wa wote. Kumbe, ubinafsi ni chanzo cha kashfa, kinzani na migongano ndani ya Kanisa! Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuwa na malengo katika maisha na kamwe wasitembee kama ”daladala iliyokatika usukani” kwa kuwa na moyo uliogawanyika na kumezwa sana na malimwengu. Kwa kukosa dira na mwelekeo wa maisha, ni vigumu sana kwa watu wa namna hii kuwa ni viongozi makini! Viongozi wa Kanisa wawe na utambulisho unaojikita katika Mapokeo ya Kanisa kwa kutambua kwamba, wao ni Wakatoliki, sehemu ya Kanisa la Kiulimwengu.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi sana kuweza kukwepa vishawishi na malimwengu yake, lakini kwa wale wanaomwamba Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku wanaweza kuzaa matunda mengi, daima wakithamini ule upendo wa kwanza kabisa waliouonesha walipokutana na Kristo katika maisha yao. Wajitahidi kuboresha maisha yao ya kiroho kwa nyenzo ambazo zimewekwa na Mama Kanisa mbele yao. Waendelee kulitajirisha Kanisa la Kristo nchini Misri kwa kuambata na kushuhudia amani iliyoachwa mbele yao na Mababa wa Umonaki, Mababa wa Kanisa waliothubutu kujichimbia Jangwani ili kusali na kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani yao katika wema na utakatifu wa maisha.

Viongozi wa Kanisa wawe ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, kwa ajili ya wokovu wa jirani zao, lakini  zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wakleri, watawa na majandokasisi wote chini ya ulinzi na tunza ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Amewaomba kumfikishia salam na matashi mema kwa waamini ambao wamekabidhiwa kwao na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu amewatakia wote matunda ya Roho Mtakatifu yaani: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi! Amewaomba kumkumbuka pia katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sala na sadaka zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.