2017-04-29 16:15:00

Vijana ni jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Misri, Ijumaa, tarehe 28 Aprili 2017 Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa washiriki wa mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa mintarafu amani ulioandaliwa na Chuo kikuu cha Al-Azhar cha Cairo nchini Misri, ameipongeza kwa namna ya pekee, Misri kuwa ni nchi ambayo ina tamaduni na hekima za kale pamoja na maagano! Ni nchi ambayo imezalisha wasomi wengi duniani na hapa ndipo panapopaswa kuwa ni chimbuko la amani, inayojikita katika majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, mintarafu asili ya binadamu, wazi na inayojenga na kudumisha mafungamano ya kijamii.

Baba Mtakatifu alipokutana na viongozi wa Serikali, Kisiasa, Wanadiplomasia pamoja na viongozi wa kidini amesema, Jamii inahitaji vyombo na wajenzi wa amani, watu wanaoweza kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao; watu wanaojikita katika huruma, upendo na udugu ili kusitisha kabisa vitendo vya kigaidi vinavyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali. Imani kwa Mungu na uzalendo kwa nchi yao ni mambo muhimu sana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini. Itakumbukwa kwamba, Misri miaka 70 iliyopita ilikuwa ni nchi ya kwanza ya Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican ili kudumisha urafiki na ushirikiano na kwamba, kuna haja ya kuendelea kuimarisha misingi hii kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu pia alikutana, akazungumza, kusali pamoja na kutoa tamko la pamoja kati yake na Papa Tawadros II. Baada ya chakula cha usiku, akiwa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Misri, alikutana na umati wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za Misri waliokuwa wanashiriki katika hija huko Cairo, Misri. Amewashukuru kwa uwepo wao na kuwaomba kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Jumamosi, ili kwa pamoja waweze kusali na kuadhimisha siku kuu, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu baada ya kusali Sala ya Baba Yetu kwa lugha ya Kiarabu, aliwaomba vijana kuwakumbuka ndugu, jamaa na marafiki zao, ili kusali kwa ajili ya kuwaombea. Baadaye, akawapatia baraka yake ya kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.