2017-04-29 15:53:00

Misri inataka kuwa ni chemchemi ya amani duniani!


Misri imekuwa na umuhimu wa pekee katika historia ya maisha ya binadamu kwani hapa ni mahali pa makutano kati ya Mashariki na Magharibi; ni nchi ambayo inarutubishwa kwa maji ya Mto Nile na kuwafunda wananchi wake kuambata busara na kuwa makini zaidi katika maisha. Misri ni nchi iliyotoa hifadhi kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu na kuwa baraka kwa wote. Hapa ni mahali ambapo Umonaki ulipata chimbuko lake. Hii ni nchi ambayo inarutubishwa kwa damu ya mashuhuda wa imani na chemchemi ya Shule ya Kitaalimungu ya Alexandria.

Haya ndiyo maneno ambayo Papa Tawadros II alipenda kuyatumia ili kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko alipomtembelea kwenye Makao yake makuu kama kielelezo cha upendo na udugu; amani na mshikamano na watu wanaoteseka kwa vita, kinzani na mashambulizi ya kigaidi. Ulimwengu una kiu ya amani na upendo ili kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu kama ilivyo hata kwa Misri ambayo imeendelea kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia, hasa vijana ambao ni amana ya taifa.

Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko usaidie kujenga na kudumisha amani kwa wananchi wote wa Misri; uendeleze umoja na mshikamano kati ya Wakristo kama ilivyokuwa kwa Mtume Petro na Mwinjili Marko; na kama ilivyotokea kwa Mwenyeheri Paulo VI na Papa Amba Shenouda III kunako mwaka 1973 kumaliza kinzani za kidini na kuambata mchakato wa umoja wa Makanisa na kuendelea kusherehekea upendo wa kidugu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox na kuendelea kushirikishana imani na chakula cha  upendo. Ni wakati muafaka wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika ushuhuda wa maisha kwa matumaini kwamba, iko siku Makanisa haya mawili yataweza kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa pamoja sanjari na kuadhimisha Noeli na Pasaka ya Bwana katika udugu na umoja.

Papa Tawadros II amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu kwa njia ya Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume bila kusahau mchango wa Wadominikani katika tafiti za kisayansi mintarafu majadiliano ya kiekumene. Maisha na utume wa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume umechangia kwa kiasi kikubwa katika maboresho ya maisha ya familia ya Mungu nchini Misri. Wanawashukuru Maaskofu wa Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia waliowawezesha waamini wa Kanisa la Kikoptik kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa katika miundo mbinu ya Kanisa Katoliki.

Papa Tawadros II anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujisadaka kwa ajili ya maskini duniani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama inavyojionesha kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi na Waraka wake wa kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” sanjari na utakatifu wa maisha ya binadamu unaobubujika kutoka katika utakatifu wa Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake. Waraka wa kitume wa “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ni dira makini na mwongozo katika maisha na utume wa Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Francisko wa Assisi pia alifanya hija na kubahatika kukutana na kuzungumza na Sultani Al Kamel wakabadilisha uzoefu na mang’amuzi ya kitamaduni na kwamba, majadiliano ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa ujenzi wa umoja kati ya watu wa mataifa na chemchemi ya matumaini mwaliko kwa Misri kuwa ni mfano wa kuigwa kwa watu kuheshimiana na kuthaminiana ili kujenga umoja, upendo na mshikamano sanjari na kukuza amani, usalama, utulivu na maridhiano mambo ambayo kimsingi ni sehemu ya utambulisho wa wananchi wa Misri kwa karne nyingi. Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mashambulizi ya kigaidi ambayo yanaweza kuonekana kana kwamba ni “dhahabu” inayosafishwa kwa watu kushuhudia kwamba, upendo na maridhiano yana nguvu zaidi kuliko hata chuki na tabia ya kulipizana kisasi; mwanga wa matumaini una nguvu zaidi kuliko giza la kukata tamaa.

Papa Tawadros II anasikitika kusema kwamba, katika kipindi cha miezi michache iliyopita Kanisa la Kikoptik na Misri katika ujumla wake, imetikiswa na mashambulizi ya kigaidi yaliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Licha ya haya yote bado wanategemea ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu na hivyo bado wanaendelea kuwa na amani, faraja na utulivu wa ndani. Katika shida na mahangaiko haya yote, Wamisri wameonesha umoja wa kitaifa katika furaha na majonzi kwa kutangaza duniani kote kwamba, vitendo vya kihalifu kamwe havitaweza kuwagawa na badala yake wataendelea kusimama kidete katika umoja, tunu msingi kwa watu wote. Misri inataka kuendelea kuwa ni chemchemi ya amani na usalama duniani na kimbilio kwa wale wanaotafuta faraja na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.