2017-04-28 07:00:00

Iweni wamissionari wa Neno na Ekaristi Takatifu: Ushuhuda wenye mvuto


Mtume wa Upendo, Mama Theresa wa Calcutta alimshangaza mwandishi wa habari mmoja aliyefika kwake kwa mahojiano maalum pale alipotaka kujua ni vipi aseme kwamba humwabudu Yesu kwa masaa 24 kila siku wakati mara nyingi huonekana akiwahudumia wahitaji, wagonjwa na fukara wa Jiji la Calcutta. Yeye alimjibu hivi: “Ndiyo, ninamwabudu Yesu masaa 24 kila siku, masaa machache mbele ya Ekaristi Takatifu ndani ya Kanisa na masaa mengine katika nafsi ya jirani yangu ninayekutana naye mahali popote.” Ibada ya Misa Takatifu, ambamo kwayo tunapata fursa ya kukutana na Kristo Mfufuka katika Neno lake na katika Ekaristi Takatifu inapaswa kuwa hai muda wote na mahali popote wakati wa maisha ya mwanadamu.

Wakati wa hitimisho la Ibada ya Misa Takatifu Padre hutualika akisema: “Nendeni na amani, mkaitangaze Injili ya Bwana au mkimtukuza Bwana kwa maisha yenu”. Ni mwaliko wa kuendelea kumfanya hai huyo tuliyekutana naye katika Neno lake na kuungana naye katika Sakramenti ya Mwili na Damu yake, Bwana wetu Yesu Kristo, Yeye aliyefufuka kutoka wafu. Katika Dominika ya tatu ya Pasaka tunatafakari juu ya muktadha huo wa mkutano wetu na Kristo katika maisha yetu ya kawaida ndani ya jamii ya mwanadamu, mkutano ambao kwa upande mmoja unanitaka mimi kuwa shuhuda wa Yeye aliyeshinda mauti kwa kufufuka katika wafu au kwa upande mwingine unaonitaka mimi kumtambua Yeye mfufuka akizungumza nami kwa njia mbalimbali.

Neno la Mungu linatupatia fursa mbili tofauti. Kwanza tunakutana na wafuasi ambao waliokuwa njiani kuelekea Emau, na katika safari yao hii njiani wanakutana na Kristo Mfufuka anayejifunua kwao katika Neno lake na kisha katika kuumega Mkate. Huu ni mfano wa ushiriki wa Mkristo katika Misa Takatifu ambayo katika sehemu zake kuu mbili yaani, Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi hukutana na Kristo mfufuka kwa kufunuliwa akili na kutiwa nguvu ya kwenda kuwa mtangazaji wa Injili Takatifu. Pili tunakutana na Mtume Petro ambaye baada ya tukio la Pentekoste akiwa na Mitume wengine anamtangaza Kristo mfufuka kwa ujasiri. Huu ni wito wa kimisionari wa kutoka nje na kwenda kumtukuza Mungu kwa maisha yetu ya kila siku. Petro akiwa amejazwa na Roho Mtakatifu anapata ujasiri na woga wote na mashaka yanamtoka. Anakutana na Kristo mfufuka ndani ya moyo wake na haoni haya kumtangaza mbele waziwazi.

Mazingira yetu yanayotuzunguka leo hii yanatuwekea mbele yetu nyakati nyingi za majaribu, mateso, kukatishwa tamaa na giza nene. Nyakati hizi ni aghalabu kutupatia fursa ya kuipenyeza imani yetu kuwa chanzo cha kujinasua na kusonga mbele kuelekea nuruni. Leo hii tunashuhudia watu wengi wanaiacha imani yao na kuyumbayumba huku na kule wakitafuta faraja. Watu hawa ni mithili ya wafuasi hawa wanaoelekea Emau. Yaliyotukia juu ya Kristo waliyafahamu kwani Neno la Mungu linatuambia kwamba “walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia”. Pengine wameamua kuuacha mji wa Yerusalemu na kugeukia mambo mengine. Wamepoteza matumaini waliyokuwa nayo juu ya Kristo, Yeye ambaye waliuona mkono wa Mungu ukitenda kazi katika nafsi yake ameishia katika namna ya kukatisha tamaa kabisa. Pia, pamoja na kupewa habari kwamba amefufuka bado walikuwa hawajakutana naye katika nafsi zao.

Hivyo Dominika hii inatupatia wajibu sisi Wabatizwa na kwa namna ya ndani zaidi inatupatia changamoto sisi tulioshiriki ibada ya Misa Takatifu na kushibishwa kwa Neno lake na Mwili na Damu yake. Ukristo wetu unatudai ushuhuda wa maisha. Ushuhuda ambao si wa kuelezea tu kwa ufundi juu ya ufufuko wa Kristo, bali ushuhuda wa maisha ambayo yatagusa nyoyo za watu wenye kukata tamaa na kumtambua Yeye aliyefufuka. Ushuhuda ambao unadhihirika katika maisha yetu ya upendo wa kindugu, wenye kushirikiana, wenye kusameheana, wenye kufarijiana, wenye kuwaonjesha wahitaji upendo wa kindugu na katika ujumla wake ni maisha yaliyopambwa na fadhila mbalimbali za kikristo. Ukristo siyo tu mkusanyiko wa mafundisho yenye weledi mkubwa ambao tunasimuliwa katika mazingira mbalimbali au zaidi tunayofafanuliwa wakati wa ibada ya Misa Takatifu; ukristo siyo tu kukesha katika ibada au kuwa na hisia za “kilokole” au kuonesha unazi katika masuala ya kiibada; ukristo siyo tu kufanya Hija katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yako au mahali pengine duniani. Ukristo ni kuhuisha hayo ambayo unakutana nayo katika maisha yako ya kila siku na kuwawezesha wengine kuyaonja na kumkiri Kristo.

Dini inahusisha imani katika nafasi ya kwanza, imani unayokuwa nayo wewe binafsi mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu. Hivyo dini inapaswa kuimarisha mahusiano yako na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anajifunua kwako kupitia mazingira ya kawaida ya kijamii. Hapa ndipo anapokupatia mwaliko wa kumsujudia na kukutana naye katika namna inayoshikika, yaani kwa mfano wa Mama Theresa wa Calcutta kumshika katika wagonjwa waliotupwa na kudharauliwa, katika maskini wanaokosa hata chembe ya unga kutuliza njaa zao, katika wajane na yatima ambao wametengwa na jamii na kudhulumiwa haki zao. Watu wa namna hii wamepoteza matumaini katika jamii na hivyo huelekeza macho yao na kilio chao kwa Mungu pekee.

Sauti ya wafuasi wawili wa Emau au mahubiri ya Petro mbele ya Wayahudi ni kwamba: “Bwana amefufuka kweli kweli”. Ufufuko wa Kristo ndiyo unaupatia maana ukristo wetu. Ukristo ni maisha ya ufufuko, fumbo ambalo limefumbatwa katika ukombozi wa mwanadamu. Kristo amekuja duniani kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa shetani na kumrejeshea tena hadhi yake. Hivyo kukiri kwetu kwamba kweli amefufuka, kiri imani ambayo inasukumwa na ukweli kwamba tumekutana naye katika Ekaristi na katika Neno lake inapaswa kujionesha katika matendo yetu ya kila siku yanayomthamini na kumpatia mwanadamu hadhi yake. Tunaalikwa kumtangaza yeye aliyefufuka kwa masaa 24 huku tukiendelea kumgusa katika jirani zetu ambao wapo katika mahangaiko na wenye kiu ya kukutana na Kristo.

Ufufuko wa Kristo unaurejeshea hadhi ubinadamu wetu. Mtume Petro anatukumbusha katika Waraka wake juu ya hadhi hiyo na wajibu wetu wa kuitunza. Yeye anatukumbusha kwamba: “tumekombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo usiofaa … bali kwa damuazizi, kama ya mwana-kondoo asiye na hila, asiye na waa, yaani, Kristo”. Na hivyo anatuhimiza kubaki katika hadhi hiyo ambayo tunashirikishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Mwili na Damu yake, yaani Ekaristi Takatifu sana. Himizo hili la kitume bado linaturudisha katika kudumisha mkutano wa mtu binafsi na Kristo, tukio tunalolionja katika Neno lake na katika kuumega mkate, katika Nyanja za maisha ya kawaida ya mwanadamu.

Kristo mfufuka anakuwa katika mwili wa utukufu, yaani mwili mtakatifu usio na doa lolote. Hii inatufunulia hadhi mpya ambayo mwanadamu anaipokea. Yeye ambaye kwa fumbo la Umwilisho anashiriki katika hali zetu zote isipokuwa hakutenda dhambi, anamkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi na kumuingiza katika katika hali ya utukufu. Mkutano wetu binafsi na Kristo katika Neno lake na katika kuumega mkate unatupatia hadhi hiyo lakini zaidi unatusukuma katika umisionari, yaani kwenda kumtangaza Kristo mfufuka ambaye tumemgusa, tumemhisi na tumemtambua katika kuumega mkate.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.