2017-04-27 16:00:00

Papa: Vijana zingatieni: sala, majiundo makini, sadaka na utume!


Jukwaa la Umoja wa Vijana Wakatoliki Kimataifa, FIAC, linaadhimisha mkutano wake wa VII kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana Wakatoliki katika utume na wote na kwa ajili ya wote”. Vijana Wakatoliki wameamua kwamba,  Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” uwe ni dira na mwongozo wa maisha na utume wao, kama sehemu ya mchakato utakaowasaidia kuwafunda vijana kuwa wamissionari mitume daima wakiendelea kujikita katika karama inayofumbatwa katika kipaji cha ugunduzi kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji mpya inayovaliwa njuga na Mama Kanisa kwa wakati huu!

Ili kufanikisha azma hii kuna haja kwanza kabisa kuwa na karama inayoongozwa na mwanga wa furaha ya Injili; kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji unaofanywa katika ngazi ya kiparokia na kijimbo; kwa kuihusisha mihimili yote ya Uinjilishaji na kwamba, walengwa ni wale wote wanaoishi pembezoni mwa mambo msingi ya maisha ya binadamu, ili kweli furaha ya Injili iweze kusimikwa kati ya watu kama kielelezo cha upendo wa Kristo kwa waja wake! Mambo makuu manne yanapaswa kuzingatiwa zaidi: sala, majiundo, sadaka na utume! Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 27 Aprili 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Jukwaa la Umoja wa Vijana Wakatoliki Kimataifa, FIAC. Majiundo yawasaidie vijana kukua na kukomaa katika imani kwa kuzingatia katekesi makini na  tafakari ya Neno la Mungu ili kujenga na kudumisha urafiki na Kristo Yesu pamoja upendo wa kidugu! Vijana wanapaswa kusali, ili kuwaombea watu ili waweze kupata mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili badala ya kujiangalia wao wenyewe Vijana wajenge utamaduni wa kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengine, kwa kutumia karama na miito yao mbali mbali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, mihimili yote ya Uinjilishaji inashirikishwa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kutambua kwamba, hii pia ni dhamana ya vijana wote pasi na ubaguzi, vinginevyo hawana sababu ya kuendelea kuwepo! Hapa kuna haja ya kupembua upya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji na majiundo awali na endelevu, ili kuwa kweli ni wamissionari tayari kusoma alama za nyakati! Vijana wanapaswa kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya Kanisa mahalia kwa kupata utambulisho wao katika Parokia na Jimbo husika, daima wakijitahidi kushiriki kikamilifu katika mipango ya kichungaji inayoandaliwa na Makanisa mahalia! Ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu unapata msingi wake kwa Makanisa mahalia!

Baba Mtakatifu anawataka vijana wote kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji kwa kuwainjilisha vijana wenzao, dhamana inayohitaji majiundo makini ya awali na endelevu, daima wakijitahidi kufanya tathmini ya mafanikio na mapungufu katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji ili kuweza kuziboresha zaidi kwa siku za usoni, daima wakiongozwa na Roho Mtakatifu anayewainjilisha, ili waweze kuinjilisha pia kwa wakati muafaka! Wajifunze kusali wakiwa wanasali! Utume huu unaweza kutekelezwa ndani na nje ya Kanisa kwa njia ya sala kama ile inayotolewa na wagonjwa.

Baba Mtakatifu anawataka Vijana Wakatoliki kushiriki kikamilifu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, ili pasiwepo hata mtu mmoja ambaye anatengwa na utume huu wa vijana, ili kushiriki kikamilifu katika nyanja zote ambazo watu wanashiriki kutoa maamuzi na utekelezaji wake. Wafungue malango ya watu li kuleta maboresho katika maisha yao, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Watu wana haki ya kutangaziwa na kushuhudiwa Habari Njema ya Wokovu, kumbe, hata vijana wanapaswa kuinjilishwa na kuinjilisha, daima wakiwa kati pamoja na watu. Kanisa haliwezi kujiweka pembeni na kusahau shida na mahangaiko ya watu, bali linapaswa kuwa ni sehemu ya maisha ya watu kwa ajili pamoja na watu! Uinjilishaji unaotekelezwa na vijana uzame katika maisha ya watu, lakini kwa kutambua kwamba, huko wanaweza kukutana na cha mtema kuni! Hizi ni changamoto anazokabiliana nazo Mama Kanisa ili kushuhudia umama wake.

Baba Mtakatifu anawaalika Vijana Wakatoliki kuonesha upendo wa Kristo kwa watu wake, kwa kujitoa kwa moyo wa ukarimu katika mchakato wa uinjilishaji, kwa kuwa huru na kumtumainia Roho Mtakatifu anayewawezesha kukua na kukomaa katika imani. Dhamana hii inatekelezwa kwa kufanya maamuzi, kushiriki, kuandamana, kuzaa matunda yanayokusudiwa na kusherehekea mafanikio yaliyofikiwa, ili kuwashirikisha wengine ile furaha ya Imani inayofumbatwa katika mchakato mzima wa uinjilishaji, kwa kujimwaga bila ya kujibakiza. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni jukwaa la kukutana na watu; kuendelea kuwa ni mihimili muhimu ya uinjilishaji kwa Makanisa mahalia, daima wakiwa waaminifu kwa utume wa Mama Kanisa katika mchakato mzima wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.