2017-04-27 15:43:00

Papa Francisko mjumbe wa amani nchini Misri!


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri kuanzia tarehe 28 – 29 Aprili 2017 inaongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri”. Licha ya changamoto za ulinzi na usalama nchini Misri hasa kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyojitokeza wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha yao nchini Misri, Baba Mtakatifu, daima ameonesha nia na uthabiti wa moyo kwenda nchini Misri kama mjumbe wa amani, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya amani na matumaini; kwa kuwatia shime wale waliopondeka na kuvunjika moyo kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa uwepo wake mwanana!

Baba Mtakatifu anataka kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekuemene ili waamini wawe kweli ni mashuhuda na wajenzi wa haki, amani na maridhiano kati yao, kwa kutambua kwamba, misimamo mikali ya kidini na kiimani inayozalisha vitendo vya kigaidi ni changamoto kubwa ya kimataifa inayopaswa kuvaliwa njuga na waamini pamoja na wapenda amani duniani! Vijana wanapaswa kuhamasisha kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, woga na wasi wasi unaopandikizwa na watu wachache ndani ya jamii kwa mafao yao binafsi! Haya ndiyo mawazo makuu yaliyomo kwenye mahojiano maalum kati ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV kama sehemu ya maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, ulimwengu huu umejeruhiwa sana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, unahitaji amani, upendo na huruma; ulimwengu unahitaji wajenzi wa amani, watu huru, wenye ujasiri wenye uwezo wa kujifunza kutokana na historia ili kujenga kesho iliyo bora zaidi badala ya kufungwa na maamuzi mbele; dunia inawahitaji wajenzi wa madaraja ya amani, majadiliano, udugu,  haki na utu wa binadamu! Kardinali Parolin anakaza kusema, Baba Mtakatifu anakwenda nchini Misri kama mjumbe wa amani.

Ulinzi na usalama ni dhamana na jukumu la serikali, kumbe, hata Wakristo ambao ni sehemu ndogo ya wananchi wa Misri wanapaswa kulindwa pamoja na kuhakikisha kwamba, mambo yote yanayopelekea misimamo mikali ya kidini na kiimani yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya majadiliano ya kidini, kwa kuzingatia elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuhakikisha kwamba, familia, shule, Kanisa na jamii katika ujumla wake zinajitahidi kurithisha tunu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wake. Vijana wafundishwe kuthamini tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii badala ya kumezwa na vitendo vya uvunjifu wa haki na amani!

Baba Mtakatifu Francisko, Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Muhammad Al Tayyib, Imam mkuu  wa Msikiti wa Al-Azhar, Cairo ni kati ya viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea umuhimu wa majadiliano ya kidini n akiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Tarehe 23 Mei 2016 Muhammad Al Tayyib alimtembelea Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican na kukazia umuhimu wa uhuru wa kuabudu, majadiliano ya kidini, amani na utulivu kati ya Wakristo na Waislam. Wote hawa wanapaswa kupewa haki na kudumisha usawa miongoni mwa raia wote wa Misri.

Elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya; uhuru wa kidini na kuabudu; umuhimu wa kuheshimu na kuzingatia uhuru wa kidhamiri kwa kuachana na wongofu wa shuruti ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuyakazia kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene sehemu mbali mbali za dunia. Elimu iwasaidie watu kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi; kukubaliana na kupokeana jinsi walivyo kwani tofauti zao ni utajiri mkubwa unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa na wote!

Kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko, Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Papa Tawadros II, ni kielelezo makini cha ushuhuda wa uekumene wa: sala na maisha ya kiroho; uekumene wa damu na huduma makini kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati ambako kumegeuka kuwa ni eneo la mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Uwepo wa viongozi hawa ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Misri kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati yao.

Ni fursa anasema Kardinali Parolin, ya kuendeleza kukazia umoja na mshikamano wa kiekumene ambao umekuwepo kati ya Makanisa haya huko Mashariki ya kati na kwamba, Wakristo watambue kwamba, Kanisa liko pamoja nao katika shida na mahangaiko yao mbali mbali kumbe hawana sababu ya kukata tamaa, bali kujizatiti zaidi katika kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kardinali Parolin anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko atahitimisha hija yake ya kitume, Jumamosi tarehe 29 Aprili 2017 kwa kukutana na kusali na waamini wa Kanisa Katoliki nchini Misri. Lengo la Baba Mtakatifu ni kuwatia shime na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake, ili waendelee kuwasha moto wa imani huko Mashariki ya kati licha ya changamoto wanazokabiliana nazo kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.