2017-04-27 16:50:00

Iweni mashuhuda wa utii kwa Mungu!


Wakristo wanayo dhamana kubwa ya kumtii Mungu kuliko wanadamu kama ambavyo Petro na mitume wenzake walivyoshuhudia kwa njia ya maisha, hata pale walipokuwa wanakabiliwa na vitisho, nyanyaso, dhuluma na kejeli katika maisha yao. Ili kweli Wakristo waweze kutekeleza dhamana hii nyeti, wanapaswa kuomba neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko ambao umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 27 Aprili 2017. Amekazia kwamba, ni Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa utii kwa Mungu na wala si kwa binadamu!

Kuhani mkuu pamoja na baraza la wazee walikuwa wamewakataza Mitume kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kwa wafu! Huu ni ushuhuda ambao ulikuwa unatolewa hata na Jumuiya ya kwanza ya Wakristo waliokuwa na moyo mmoja na roho moja, wakashirikiana na kugawana kile walichokuwa nacho. Mitume wakaendelea kushuhudia ufufuko wa Kristo kwa nguvu na neema nyingi. Kama ilivyo kawaida katika “msafara wa Mamba, Kenge hawakosi”, ndivyo ilivyokuwa hata kwa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ambamo walikuwepo pia akina Anania na Safira mkewe, waliouza mali yao na kuficha sehemu ya mapato kwa kuwadanganya Mitume, lakini wakakiona cha mtema kuni anasema Baba Mtakatifu.

Hata leo hii kuna watu ambao wanashutumiwa na kudhihakiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kama ilivyokuwa hata kwa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Wagonjwa walipelekwa kwa mitume ili kuwaombea na kuwawekea mikono yao wapate kupona! Mtume Petro aliyekuwa na makovu ya kumkana Kristo Yesu mara tatu, wakati huu anatoka kifua  mbele pasi na woga, akiwa amejaa nguvu ya Roho Mtakatifu na kusema, wao imewapasa kumtii Mungu kuliko wanadamu! Huu ndio ushuhuda wa utii kwa Mungu unaopaswa kutekelezwa na Wakristo wote kama alivyofanya Kristo Yesu alipokuwa bustanini Getsmane, alipojiachilia mikononi mwa Baba yake wa mbinguni ili kuweza kutekeleza mapenzi yake!

Baba Mtakatifu anasema, hii ni neema kutoka kwa Roho Mtakatifu ambayo waamini wanapaswa kuiomba ili kweli waweze kuwa watiifu sanjari na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Ni Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kutubu na kumwongokea Mungu, anayeweza kuwageuza na kuwa kweli ni mashuhuda wa utii kwa Mungu. Utii kwa Mungu una matokeo yake ambayo ni madhulumu, nyanyaso na hatimaye kifo! Msalaba daima utaendelea kuwaambata wakristo katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili kuwasaidia kuboresha maisha yao kwani changamoto za maisha wanazo daima mbele yao. Ili kuweza kuwa kweli ni mashuhuda wa utii kwa Mwenyezi Mungu, waamini wanapaswa kusali daima na kujitambua kwamba, wao ni wa dhambi mbele ya Mungu. Wawe na ujasiri wa kumwomba Roho Mtakatifu neema na baraka kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa utii kwa Mungu, daima wakiwa tayari kukabiliana na dhuluma, nyanyaso hata na kifo kutokana na msimamo wao wa maisha, kwani daima Roho Mtakatifu atawasaidia katika shida na mahangaiko yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.