2017-04-26 13:05:00

Sera na mikakati ya kisiasa na kiuchumi itoe kipaumbele kwa binadamu!


Sera na mikakati ya kiuchumi inaonekana kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vitu na faida kubwa na kumweka mwanadamu, mahitaji yake msingi na utu wake, pembezoni kama gari bovu! Dunia inaweza kubadilishwa kwa kujikita katika wema, upendo, mshikamano na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Kimsingi, hiki ni kiini cha ujumbe kwa njia ya video uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, usiku wa kuamkia, Jumatano tarehe 26 Aprili 2017 kwa washiriki wa mkutano TED 2017 unaowajumuisha wadau kutoka katika masuala ya kiuchumi, kisayansi na kitamaduni kutoka sehemu mbali mbali mbali za dunia.

Kauli mbiu ya mwaka huu 2017 ni “Wewe ndiyo kesho”! Ili kuleta mabadiliko ulimwenguni kuna haja ya kujenga utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana na wengine, lakini zaidi kwa kuwasikiliza na kujibu kilio cha maskini, tayari kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kujielekeza katika mambo msingi ya maisha ya mwanadamu yanayosimikwa katika: udugu na mshikamano ili kupambana na ubinafsi, vita, chuki na mipasuko ya kijamii mambo yanayodharirisha utu na heshima ya binadamu!

Kuna haja ya kuwa na sera na mikakati makini ya kiuchumi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Ili kuweza kutekeleza dhamana hii, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kushirikiana na kushirikishana kwani hakuna mtu anayeweza kuishi na kujimudu peke yake kama kisiwa. Ustawi na maendeleo ya binadamu kwa siku za usoni yanajengwa na kudumishwa kwa njia ya mshikamano wa dhati! Watu wawe na ujasiri wa kusafisha dhamiri zao ili kuondokana na mawazo mgando na maamuzi mbele ili kuganga na kuponya majeraha ya vita na kinzani za maisha, tayari kusamehe na kusahau ili kuzima moto unaowaka ndani mwao ili yabaki majivu peke yake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mshikamano na udugu vinapaswa kuwa ni sehemu muhimu sana wa sera, mikakati na maamuzi ya kiuchumi kwa kujikita zaidi katika mchakato unaopania kujenga na kudumisha usawa kati ya watu sanjari na mafungamano ya kijamii. Watu wawe na ujasiri wa kuguswa na mahitaji pamoja na mahangaiko ya jirani zao kwa kukazia mshikamano wa kidugu, msamihati ambao kwa wengi unaonekana kana kwamba, umepitwa na wakati!

Sera za kisiasa, kiuchumi na kisayansi zijitahidi kujikita katika mchakato wa maboresho ya mahusiano kati ya watu na nchi zao. Elimu ifumbate udugu unaomwilishwa katika mshikamano ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Binadamu na mahitaji yake msingi, awe ni sababu ya mshikamano wa kiteknolojia, lakini kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu, mara nyingi vitu na faida kubwa vimepewa kipaumble cha kwanza! Mshikamano ni maamuzi yanayobubujika kutoka katika undani wa mwanadamu pamoja na changamoto zake kwa kutambua kwamba, maisha ni zawadi ya upendo inayotoa maana ya maisha, kiasi cha kumsukuma mtu kuwajali pia jirani zake. Upendo daima unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu na kamwe usibaki ukiwa unaelea kwenye ombwe tu! Mfano wa Msamaria mwema anasema Baba Mtakatifu Francisko ndiyo hali inayowasibu walimwengu kwa nyakati hizi. Kuna watu wanateseka na kunyanyasika kutokana na uchu wa mali na madaraka; kuna watu wanaojitenga na wengine kiasi hata cha kushindwa kuwatekelezea hata yale mambo msingi ambayo yako kwenye uwezo wao; hawa ndio wale wanaowageuzia kisogo watu wenye matatizo na magumu ya maisha.

Watu wawe na ujasiri wa kuwasaidia wengine kadiri ya uwezo na nafasi zao kwa kuiga mfano bora kutoka kwa Mama Theresa wa Calcutta. Wema na upendo ni tunu zinazobubujika kutoka katika undani wa mwanadamu. Katika giza na ubaya wa moyo unaojionesha kwa namna ya pekee katika vita, kila binadamu anaweza kuwa ni mshumaa unaofukuza giza katika maisha ya watu. Haya ndiyo matumaini yanayopaswa kuangaza na kuwamulikia watu wanaotembea katika giza, ili kuona yale yaliyopita, kuganga mambo ya wakati huu na kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.

Upendo na wema anasema Baba Mtakatifu Francisko, ni chachu ya mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu kwani tunu hizi zinamwezesha mtu kusikiliza kwa makini na kujibu kilio cha maskini sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wema na huruma ni lugha inayotumiwa na watoto kupata mahitaji yao msingi. Ni hali ya kujinyenyekesha kama alivyofanya Mwenyezi Mungu katika Fumbo la Umwilisho, akawa ni mfano bora wa kuigwa kwa  kwa watu jasiri na wenye nguvu; huruma ni kielelezo cha nguvu!

Baba Mtakatifu anawaalika watu waliopewa dhamana na madaraka kutambua kwamba, nguvu hii inapaswa kutumika kwa ajili ya huduma na kutenda mema kwa jirani. Viongozi wanapaswa kuonesha mfano bora wa unyenyekevu na huruma ambayo ikimwilisha katika maisha ya watu inakuwa ni huduma tayari kutenda mema. Ustawi na maendeleo ya binadamu kwa siku za usoni uko si tu mikononi mwa wanasiasa, bali pia wachumi na wapanga sera bila kusahau makampuni makubwa makubwa. Kesho ya binadamu inafumbatwa katika utambuzi wa jirani yako kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha yako!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.