2017-04-26 16:10:00

Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar!


Sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zimefanyika 26 Aprili 2017 mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli. Ni siku ambayo Tanganyika na Zanzibar ziliungana na  Tanzania ikazaliwa. Ni sikukuu ya aina yake kwa mwaka huu kwasababu ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania sikukuu hii kufanyika kitaifa mjini Dodoma. Uwanja umefurika na wanachi ambao waiimba wimbo wa taifa wakiongozwa na amiri mkuu Rais Magufuri. Gwaride la kijeshi, ngoma na burudani kama kawaida ya sikukuu zote za kitaifa nchini Tanzania, zimeurahisha na kuchangamsha watazamaji kutoka pande nyingi za Taifa.

Huo ndiyo uzalendo mkubwa kwa nchi ya Tanzania ambayo bado inataka kuendeleza kuonesha upendo na mshikamano kwa miaka sasa 53 tangu kuunganika kwake.Pamoja na hayo bado kuna changamoto  nyingi sana , na hasa zile zinatokana kwa namna moja au nyingine ni ukosefu wa kushirikisha kwa maana ya kutembea pamoja ili kuweza kupata kujikwamua katika kendeleza nchi kwani ubinafsi ukajikita mizizi yake.Kutokana na ubinafsi huo umeipelekea nchi ya Tanzania kwa miaka sasa uwepo na mgawanyiko wa watu wenye utajiri mkubwa na walio masikini zaidi.Ili kila mmoja atafute  kwa manufaa binafsi, matukio mengi yasiyo stahili katika jamii yamejitokeza.Kwa mifano halisi ndiyo maana hata kauli mbiu ya sherehe za kutimiza miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa mwaka 2017 ni ; Miaka 53 ya Muungano; Tuulinde na Kuuimarisha, Tupige Vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii,”

Hiyo ni wazi na pia kuwa changamoto inayohitaji kila mtazania, asiwe mtazamaji maana ni muhusika moja kwa moja kwa hali moja au nyingine.Pamoja hayo bado changamoto kubwa za  kiuchumi, elimu afya ambavyo vinahitaji nguvu ya pamoja katika kuindeleza nchi ya Tanzania, ambayo kwa miaka mingi imejivunia uhuru wake, na watu wake.Inasikika majuvuno hayo ya tanzania katika nyimbo za watunzi wetu wa zamani, na hivyo kauli mbiu ya mwaka huu ni kama kutoa wito ya kwamba kujivunia nchi yetu isibaki katika nyimbo bali uwe ni uhalisia wa kila mtanzania , anaye jiita mzalendo wa tanzania , mwenye kupenda amani,mshikamano wa kindugu kwa watu wote na hasa katika kujikita kwenye ulinzi wa amani, utetezi wa watoto yatima na wanawake, utetezi wa walemavu wa ngozi, wazee , watu walio tengwa au kunyapaa, kuwatembelea wafungwa, utetezi wa haki msingi.

Haya ni baadhi ya mambo machache ambayo kila mtazania anawajibika, hapaswi kukwepa, kwani raia lazima wawajibika kuwa wazi , wafichue maovu, wafanye kazi kwa bidii kwa ajili ya manendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania na kwa ajili ya watu binafsi.Hiyo ndiyo moyo wa waasisi wetu Mwalimu Nyerere na Karume walivyokuwa wanataka.Nchi yoyote yenye rahia wa kupenda nchi yake kwanza, lazima ataitete na kuilinda, ni wajibu wetu wote.

Historia fupi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar:Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa mnamo tarehe 26 Aprili, 1964 kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja). Tanganyika ilikuwa ni mwendelezo wakoloni la Ujerumani, utawala wa Waingereza kwa Mamlaka ya Umoja wa Mataifa, Himaya ya Umoja wa Mataifa chini ya utawala wa Uingereza na mwisho Taifa huru kuanzia mwaka 1961 ndani ya nchi za Jumuiya ya Madola. Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkataba huu wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar. 

Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi hapo tarehe 26 Aprili, 1964 na mnamo tarehe 27 Aprili, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano. Sheria za Muungano zilitoa tamko la Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 4 kwamba:“Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitalazimika, baada ya kuungana na siku zote baada ya kuungana, kuunganishwa kuwa Dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ (Ibara ya 4 Sheria za Muungano)” Jina hili la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadae mnamo tarehe 28 Oktoba, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.

MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE, DUMISHA UMOJA NA AMANI, 
Na Sr Angela Rwezaula 
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.