2017-04-25 14:31:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa familia ya Mungu nchini Misri!


Baba Mtakatifu Francisko wakati  huu wa maandalizi ya hija yake ya kitume nchini Misri ametuma ujumbe wa matashi mema kwa familia ya Mungu nchini humo, akiitakia amani kama kielelezo cha furaha kuu iliyoko moyoni mwake wakati huu anapoendelea kujiandaa kwa ajili ya kutembea nchi yao ambayo ina utajiri mkubwa wa utamaduni, iliyobahatika kupata Mto Nile, nchi angavu na inayojikita katika ukarimu. Misri anaendelea kusema Baba Mtakatifu ni mahali ambapo Mababa wa imani na Manabii waliishi na hapa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu, mwingi wa wema na huruma aliweza kuifanya sauti yake kusikika!

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza akisema, ana furaha kubwa sana moyoni mwake kuwatembea kama rafiki, mjumbe wa amani na hujaji katika nchi ambayo takribani miaka elfu mbili iliyopita iliweza kutoa kimbilio na hifadhi ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iliyokuwa inakabiliana na vitisho vya Mfalme Herode. Baba Mtakatifu anasema, anayofuraha sana kutembelea nchi ambayo iliwahi kutembelewa pia na Familia Takatifu. Anawashukuru kwa kumwalika kutembelea Misri ambayo wao wanaiita “Umm il Dugna” yaani “Mama wa Ulimwengu”. Anamshukuru kwa namna ya pekee kabisa Rais wa Misri, Papa Tawadros II Mufti Mkuu wa Msikiti wa Al-Azhar pamoja na Patriaki wa Kanisa Katoliki la Kikoptik.

Baba Mtakatifu anasema, ni matumaini yake kwamba, hija yake ya kitume itakuwa ni kwa ajili ya kuwafariji na kuwatia shime Wakristo wote huko Mashariki ya Kati; anataka kuwashirikisha ujumbe wa urafiki kwa kuwaheshimu wananchi wote wa Misri na Ukanda huo mzima. Anasema, ana ujumbe wa udugu na upatanisho kati ya watoto wote wa Abrahamu, Baba wa imani, hasa zaidi, waamini wa dini ya Kiislam, ambamo, Misri inapewa kipaumbele cha pekee. Ni matumaini yake kwamba, uwepo wake nchini Misri utasaidia kusongesha mbele majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam sanjari na majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Kanisa la Kikoptik.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, ulimwengu huu umejeruhiwa sana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, unahitaji amani, upendo na huruma; ulimwengu unahitaji wajenzi wa amani, watu huru, wenye ujasiri wenye uwezo wa kujifunza kutokana na historia ili kujenga kesho iliyo bora zaidi badala ya kufungwa na maamuzi mbele; dunia inawahitaji wajenzi wa madaraja ya amani, majadiliano, udugu,  haki na utu wa binadamu! Baba Mtakatifu anasema anapenda kuikumbatia familia yote ya Mungu nchini Misri na kuiombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuwabariki na kuilinda nchi yao dhidi ya ubaya wowote! Mwishoni, anawaomba pia wao kumwombea amewashukuru kwa kusema, Shukrani wa Tahiai Misr. Asanteni sana, Idumu Misri!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.