2017-04-25 15:00:00

Papa Francisko mjumbe wa amani nchini Misri


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri inaongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri” itaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 28- 29 Aprili 2017. Baba Mtakatifu anakwenda nchini Misri kama mjumbe na shuhuda wa amani katika hija yake ya kumi na tisa kimataifa ambayo ina umuhimu wa pekee sana ukizingatia kwamba, hivi karibuni, kumekuwepo na mashambulizi ya kigaidi nchini Misri yaliyoplekea maafa makubwa kwa wananchi wa Misri. Baba Mtakatifu atatumia gari la kawaida wakati wote wa hija yake ya kitume nchini Misri ili kukutana na kuzungumza na watu kama mjumbe wa amani!

Baba Mtakatifu anatembelea Misri ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani; anapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo nchini Misri ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Haya ni mambo msingi anasema Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican yanayoipamba hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri. Kuna umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Misri wanaosubiri kwa hamu kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Misri inakuwa ni nchi ya 27 kutembelewa na Papa Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anatembelea Misri kwa mwaliko wa Rais  Abdel Fattah Saeed Hussein Khalil el-Sisi pamoja na viongozi wa kidini nchini Misri. Hawa ni Papa Tawadros II wa Kanisa la Kikoptik nchini Misri, Imam mkuu  wa Msikiti wa Al-Azhar, Cairo, Sheikh mkuu Muhammad Al Tayyib. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwasili Cairo nchini Misri majira ya saa 8:00 mchana na kupokelewa na wenyeji wake na hatimaye, kwenda Ikulu ya Misri kumtembelea Rais. Baadaye atamtembelea Imam mkuu nyumbani kwake na wote wawili wataondoka kuelekea kwenye mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa kuhusu umuhimu wa kujenga na kudumisha amani duniani. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anatarajiwa pia kushiriki katika mkutano huu wa kimataifa, ili kukazia umuhimu wa majadiliano ya kidini katika kujenga na kukuza misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa mataifa!

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, baada ya mkutano huu wa majadiliano ya kidini kimataifa, Baba Mtakatifu Francisko atakutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, kisiasa, wanazuoni pamoja na mabalozi wanaoziwakilisha nchi na mashirika yao nchini Misri. Ziara hii ya Baba Mtakatifu Francisko itafungua pazia jipya la majadiliano ya kiekumene kwa kukutana na Papa Tawadros II. Haya ni majadiliano ya uekumene wa dam una huduma makini; uekumene wa sala na maisha ya kiroho. Mkutano huu utafanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro, kwani Kanisa kuu hivi karibuni liliharibiwa vibaya sana kutokana na mashambulizi ya kigaidi.

Viongozi hawa wawili watasali kwa pamoja ili kuwaombea Wakristo wote waliopoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi sanjari na misimamo mikali ya kidini! Hapa mkazo ni uekumene wa damu kama njia ya ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu atahitimisha siku yake ya kwanza na kuelekea kwenye makao makuu ya Ubalozi wa Vatican nchini Misri, huko atakutana na watoto wanaosoma kwenye shule ya Wacomboni mjini Cairo. Baada ya chakula cha usiku, Baba Mtakatifu atakutana na kusalimiana na vijana wanaofanya hija ya maisha ya kiroho nchini Misri.

Baba Mtakatifu Francisko ataianza Jumamosi ya tarehe 29 Aprili 2017 kwa kukutana, kusali na kuzungumza na Jumuiya ya Wakatoliki nchini Misri, ambayo kimsingi bado inabaguliwa sana. Majira ya saa 4:00 asubuhi, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya tatu ya Pasaka kwenye Uwanja wa Jeshi la anga na baada ya Misa, kama kawaida atazunguka uwanjani kusalimiana na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema watakaokuwa wamehudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu. Baadaye atapata chakula cha mchana na Baraza la Maaskofu Katoliki Misri na kabla ya kuondoka, atakutana na kuzungumza na Wakleri, watawa na Majandokasisi. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega ili kukujuza mambo msingi yatakayokuwa yanajiri wakati wote huu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.