2017-04-18 12:18:00

Maaskofu Katoliki Ghana: Iweni mabalozi wa haki, amani na upatanisho!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana katika ujumbe wake Pasaka kwa Mwaka 2017 kwa Familia ya Mungu nchini humo, linawatakia heri na baraka, amani na upatanisho kati yao na jirani, Mwenyezi Mungu pamoja na kazi ya uumbaji. Askofu mkuu Philip Naameh, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana anasema amani ni kito chenye thamani kubwa, ni tunda la haki na upendo wa dhati na kamwe vurugu si jibu la kutafuta amani ya kweli. Amani ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu! Amani ni zawadi ya Kristo Mfufuka kwa waja wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana likifanya rejea kwa Mtakatifu Toma, mwenye imani haba, ambaye hakuamini kuhusu ufufuko wa Kristo na kutaka kuona ushuhuda kwa kugusa Madonda yake ya Matakatifu, linasema hiki ni kielelezo cha utepetevu wa imani kiasi hata cha kushindwa kuamini ushuhuda uliokuwa umetolewa na mitume wengine waliobahatika kukutana na Yesu “mubashara”. Maaskofu Katoliki wa Ghana wanasema, hiki ni kielelezo cha mapambano ya imani yanayoendelea kujikita katika maisha ya familia ya Mungu nchini Ghana. Kristo Mfufuka alisaidia kurejesha imani, amani, upendo na mshikamano kati ya wafuasi wake, baada ya kutikiswa kwa kiasi kikubwa na kashfa ya Msalaba!

Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho, haki na amani; kwa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika utekelezaji wa sera, maamuzi na mikakati ya utekelezaji wa haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Ghana, kamwe wasikubali kushindwa kutokana ubinafsi wao! Wananchi wawe tayari kusameheana, tayari kumwilisha ujumbe wa Mtakatifu Paulo, mtume na mwalimu wa mataifa anayewataka kuwa kweli ni mabalozi wa upatanisho, umoja, upendo na mshikamano. Waamini wawe wepesi kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Wawe tayari kuifia dhambi na kuambata utakatifu wa maisha!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana linakaza kusema, ujumbe wa Pasaka ya Bwana una umuhimu kwa familia nzima ya Mungu nchini Ghana kama taifa, changamoto na mwaliko wa kuondokana na utamaduni wa kifo na mambo yale yote yanayowapelekea watu katika kifo. Kama taifa wanapaswa kupambana na magonjwa, umaskini, njaa pamoja na kudhibiti ajali barabarani ambazo zimekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wananchi wote wasimame kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote.

Sera na mikakati makini ya huduma bora ya afya isaidie kuokoa maisha ya watoto wadogo wanaofariki dunia wakiwa chini ya umri wa miaka mitano. Kama taifa, wananchi washikamane kupambana na mmong’onyoko wa maadili na utu wema; kwa kukataa kishawishi cha rushwa na ufisadi; kwa kuheshimu na kushuhudia Injili ya uhai; kwa kuwaheshimu wazee na vikongwe pamoja na kuendelea kujielekeza katika uponyaji wa madonda ya kinzani na utengano; kwa kujielekeza katika upatanisho, umoja, upendo na mshikamano wa kifamilia na kitaifa. Ujumbe wa Kristo Mfufuka uwe ni chachu ya mabadiliko si tu kwa waamini bali kwa familia nzima ya watu wa Mungu nchini Ghana, kwani kitu chema unakula na jirani yako! Ujumbe wa Pasaka ni amani kwenu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.