2017-04-17 16:50:00

Tuwe ishara ya Kristo Mfufuka katika ulimwengu wenye matatizo!


Jumatatu ya Sikukuu ya Pasaka, inaitwa Jumatatu ya malaika, Liturujia inatoa habari ya ufufuko ikiitangazwa ya kwamba Bwana amefufuka Aleluya. Katika Injili ya siku ya Jumatatu, tunaweza kuona mwangwi wa maneno ya Malaika aliyo waeleza wanawake kaburini. “ Haraka nendeni mkawambie mitume wake, amefufuka kutoka wafu”( Mt 28,7).Ni maneno ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Mbingu, ikiwa ni Jumatatu ya tarehe 17 Aprili 2017 ambapo Kanisa katoliki, likiwa bado linasheherekea siku ya Pili tangu  ufufuko wa Bwana Yesu kutoka katika wafu.

Baba Mtakatifu amesema ujumbe huo tuusikie ya kuwa unatualika hata sisi moja kwa moja, kufanya haraka kwenda kutangaza kwa wanaume na wanawake wa nyakati zetu , ujumbe wa furaha na matumaini. Matumaini na uhakika wa matumaini hayo ni kwasababu, baada ya machweo siku ya tatu, msulibiwa amefufuka na ndiyo neno la mwisho  na siyo la kifo bali la maisha! Huo ndio uhakika wetu ya kwamba neno la mwisho siyo kaburi na wala si kifo  bali ni maisha tu.  Kwa njia hiyo turudie kwa nguvu kusema Kristo amefufuka , kwasababu Yeye ameshinda mauti kaburini na kutoa maisha mapya.

Katika matukio hayo yanayounda habari moja ya kweli katika historia ya ulimwengu, tunaalikwa kuwa watu wapya kwa njia ya Roho na kushuhudia thamani ya maisha.Ndiyo hayo  maisha ambayo Baba Mtakatifu Fransisko amesisitiza kuanzia  machweo ya jua: “tutakuwa wanaume na wanawake wa ufufuko iwapo tutaweza kutoa ushuhuda kati ya matukio mengi yanayoikumba dunia, kati ya malimwengu yanayosababisha kwenda mbali na Mungu; na iwapo tutatambua kutoa ishara ya mshikamano;  na ishara ya kukaribisha; iwapo tutakuwa na hamu ya amani ya ulimwengu mzima inayo zingatia utunzaji bora wa mazingira bila uharibifu. Hizo ni ishara za pamoja , lakini pia zinazo endelezwa na kuhimarishwa kwa imani ya Bwana mfufuko. Ishara hizo pia zinaweza kuwa mwafaka wa hali ya juu ya uwezo wetu ila ni kwasababu Kristo ni mzima, ni Kristo anayetenda katika historia kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu, analipiza dhambi zetu, anamfikia kila binadamu na kumpa matumaini na yeyote ambaye ameonewa na mateso.

Baba Mtakatifu Fransisko amemalizia mahubiri yake akisema: “Bikira Maria shuhuda wa ukimya wa kifo na ufufuko wa mwanae Yesu, atusaidie kuwa ishara wazi za Kristo katika matukio ya dunia ili wanaoteseka katika matatizo ya dunia, wasibaki waathirika na kushindwa hadi kufikia kujisalimisha, bali wapate msaada na utulivu kutoka kwetu sisi. Mama Maria aweze kutusaidia kuamini kwa nguvu  zote ufufuko wa Yesu. Yesu mfufuka, anayeishi  kwetu na katika makazi yetu, na hilo ndilo fumbo la ukombozi, ule uwezo wake wa kuadili mioyo na maisha. Kwa njia hiyo awaombee kwa namna ya pekee leo hii Jumuiya zote za kikristu sehemu mbalimbali za dunia zinazotesika na kusongwa na matatizo ,wapate kuwa na ujasiri wa ushuhuda katika hali hiyo ngumu”. Baba Mtakatifu ameongeza kwa kusema,  katika mwanga  na furaha ya Pasaka tuungane na Mama Maria katika sala ambayo kwa siku hamsini hadi Siku kuu ya Pentekoste, Sala ya Malkia wa mbingu  itachukua nafasi ya Sala ya Malaika wa Bwana.

Mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Baba Mtakatifu Francisko ametoa salam zake kwa mahujaji wote walio unganika katika viwanja vya Mtakatifu Petro, wakiwa ni kwa familia mbalimbali, makundi mbali mbali ya parokia , vyama na watu binafsi kutoka nchini Italia na kutoka pande zote za dunia. Kwa kila mmoja amewatakia matashi mema ya heri , kuwana  utulivu  kwa kipindi chote cha siku nane ya furaha ya ufufuko wa Bwana. Aidha amewataka watu wote kutafuta kila  fursa yoyote katika kushuhudia  amani ya Bwana Mfufuka. Amemalizia kwa kuwatakia Pasaka njema wakati huo akiomba hata sala kwa ajili yake.

Sr Angela Rwezaula.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.