2017-04-16 15:03:00

Papa Francisko: Kristo Mfufuka ni chemchemi ya matumaini mapya!


Mkesha wa Pasaka ni tukio ambalo limesheheni utajiri mkubwa wa Fumbo la Ukombozi, pale ambapo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo alipoamua kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Mkesha wa Pasaka ni mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Mama Kanisa. Ni mkesha wenye utajiri mkubwa wa Mafumbo ya maisha na utume wa Kanisa unaodhihirishwa kwa namna ya pekee na alama mbali mbali zinazotumika.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 15 Aprili 2017, ameadhimisha Mkesha wa Pasaka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kubariki Mshumaa wa Pasaka na hatimaye kuongoza maandamano kuingia kwenye Kanisa kuu. Mkesha umepambwa kwa Liturujia ya Neno la Mungu kuonesha mchakato wa Fumbo zima la Ukombozi tangu Agano la Kale na hatima yake ni Fumbo la Pasaka! Ameongoza Liturujia ya Ubatizo, kwa waamini kurudia tena ahadi zao za ubatizo na wakatekumeni kumi na mmoja kutoka sehemu mbali mbali za dunia kupokea Sakramenti ya Ubatizo, kwa kuzaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu na hatimaye, kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, tayari kumshudia Kristo kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ameonesha kwa namna ya pekee kabisa, uchungu wa akina Mariamu  waliojihimu mapema asubuhi siku ya kwanza ya juma kwenda kulitazama kaburi, uchungu kwa watu ambao wamekosewa haki msingi katika maisha! Haya ni machozi ya wanawake wenye huruma wanaomboleza kifo cha Kristo Yesu mkombozi wa dunia anayewakirimia walimwengu matumaini mapya. Ni wanawake waliokuwa wanaomboleza kwa kuondokewa na mpendwa wao, tofauti kabisa na Mitume wengine waliotimua mbio na kutokomea mafichoni! Lakini wanawake walionesha ujasiri na moyo mkuu, wakamsindikiza Yesu katika Njia ya Msalaba, wakashuhudia akiinamisha kichwa na kukata roho Msalabani. Wanawake wakaandamana na Yosefu wa Arimathaya kwenda kumzika Yesu, kielelezo cha watu wenye ujasiri wanaothubutu kusonga mbele kwa imani na matumaini licha ya magumu na changamoto za maisha zinazowaandama.

Baba Mtakatifu anasema hawa ndio wale wanaoelemewa na umaskini, dhuluma na nyanyaso; ndio wakimbizi na wahamiaji ambao wamegeuka kuwa yatima pasi na makazi wala familia. Ni nyuso za watu wanaoelemewa na upweke hasi; wanawake wanaowalilia watoto wao wanaomezwa kwa matumizi haramu ya dawa za kulevya, rushwa, ufisadi na ubinafsi unaowapoka watu wengi matumaini katika maisha. Wanawake hawa ni kielelezo cha ukiritimba usiokuwa na mvuto wala mashiko; ukiritimba usiopenda kuona mageuzi; hawa wote ni mfano wa watu wote ambao utu wao unatundikwa Msalabani kila kukicha!

Nyuso za wanawake hawa zimo nyuso za watu wote pamoja na uso wako anasema Baba Mtakatifu.  Uaminifu wa Mungu ni jambo lenye uhakika kabisa, ingawa bado hali ya kukosa uaminifu inatawala katika maisha ya waamini wengi; watu wanaotaka kuendeleza mapambano ambayo hayana mashiko hata kidogo, wanataka kuendelea kuishi makaburini huku wakiwa wanaendelea kuchanganyikiwa na hatimaye, kuzima matumaini yanayobubujika kutoka kwa Mungu. Watu waliokata tamaa wanakufa na Kristo pamoja na kuzika matumaini yao. Wanawake wale waliingiwa na furaha kupita kiasi walipoambiwa wasiogope! Amefufuka kama alivyosema! Yule aliyeteswa, akafa na kuzikwa kaburini amefufuka na ni mzima kabisa, chemchemi ya matumaini mapya yanayoleta mabadiliko makubwa katika maisha ya binadamu. Yesu Mfufuka anabomolea mbali kuta za utengano zinazowatenganisha watu na uhalisia wa maisha; watu wanao tafuta uhakika na usalama wa maisha yao; wenye uchu wa mali na madaraka kiasi hata cha kupoka utu na heshima ya wengine. Kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwakirimia walimwengu huruma yake kwa njia ya ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mkesha wa Pasaka ni changamoto na mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kama walivyofanya akina Mariamu, wanawake wa shoka na mashuhuda wa ufufuko wa Kristo! Kifo kamwe hakina neno la mwisho. Wakristo wanapaswa kutangaza, kufunua na kushuhudia kwamba, kweli Kristo Yesu amefufuka kutoka kwa wafu, tumaini la wale ambao utu na heshima yao vimwekwa rehani, ushuhuda wa Wakristo wa kweli! Huu ndio upya wa maisha unaoletwa na Kristo Yesu; huruma na upendo wake unaleta mabadiliko katika udhaifu wa maisha ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.