2017-04-16 15:24:00

Kumbu kumbu ya Miaka 90 tangu kuzaliwa kwa Papa Mstaafu Benedikto XVI


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Siku kuu ya Pasaka, Jumapili tarehe 16 Aprili 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Sala ya waamini, amemkumbuka pia Papa mstaafu Benedikto XVI anayeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 90 tangu alipozaliwa, shuhuda wa imani katika Fumbo la Ufufuko. Kanisa limemwombea ili kweli Yesu Mfufuka ambaye yuko hai kabisa, aweze kumbariki, kumkirimia uwepo wake mwanana na kumtunza katika urafiki wake.

Kumbu kumbu hii anasema Askofu mkuu Georg Ganswein, Mkuu wa nyumba ya Kipapa itaadhimishwa rasmi, Jumatatu ya Pasaka, katika Monasteri ya “Mater Ecclesia” iliyoko mjini Vatican ambako, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anaendelea kutafakari na kusali kwa ajili ya Kanisa la Kristo! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI baada ya kung’atuka kutoka madarakani kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alipenda kuwa na maisha ya faragha, lakini kwa kupanda kwenda Mlimani kama alivyofanya Musa ili kusali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, kadiri ya nguvu na uwezo ambao Mwenyezi Mungu anaendelea kumkiria katika huruma na upendo wake!

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI muda wake mwingi anautumia kwa ajili ya sala, tafakari, kuandika, kukutana na kusalimiana na wageni mbali mbali wanaomtembelea pamoja na kusikiliza muziki, kwani muziki, jamani ni sabuni ya roho wanasema waswahili. Zaidi anapenda kuutumia muda huu kwa ajili ya kujiandaa kukutana na Kristo Yesu, hakimu mwenye huruma na mapendo baada ya kumaliza safari yake hapa duniani! Anatembea kwa shida na uzee nao unaendelea kubisha hodi pasi na subira. Ni kiongozi asiyelalama hata kidogo, upole na unyenyekevu wa moyo vimekuwa ni silaha kubwa katika maisha yake. Ni kiongozi mwenye imani thabiti na anayependa kuwashirikisha na kuwarithisha wengine zawadi hii kwa moyo wa ukarimu. Uhusiano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Papa Mstaafu Benedikto XVI ni mzuri, kwani wanawasiliana na kutembeleana mara kwa mara panapokuwepo na sababu msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.