2017-04-14 14:23:00

Papa Francisko awataka wafungwa kuwa mashuhuda wa upendo kati yao!


Alhamisi kuu Jioni, Mama Kanisa ameadhimisha kumbu kumbu ya siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na daraja takatifu pamoja na kuwaosha Mitume wake miguu, alama ya huduma makini inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni, 13 Aprili 2017 katika Ibada ya Misa Takatifu ya Karamu ya Mwisho, ametembelea Gereza la Paliano lililoko mjini Frosinone, Jimbo Katoliki la Palestrina, Italia na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Katika Ibada hii ambayo imehudhuriwa na wafungwa ambao wengi wao wanatumikia kifungo cha maisha na baadhi yao wanatarajiwa kumaliza adhabu yao kati ya mwaka 2019 hadi mwaka 2073 amewaosha miguu wafungwa kumi na wawili. Kati yao kulikuwepo wanawake watatu na kijana mmoja wa dini ya Kiislam ambaye amekubali kuongoka na sasa anaendelea na mafundisho ya katekesi, tayari kubatizwa kwa wakati muafaka.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaambia wafungwa hawa kwamba, Yesu hali akiwa anatambua kwamba, saa yake imewadia ya kutoka katika ulimwengu huu na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni; alitambua pia kwamba, alikuwa amesalitiwa na Yuda Iskariote kwa vipande thelathini vya fedha, lakini aliwapenda watu wake, tena akawapenda upeo! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopenda kwa dhati, kiasi hata cha kusadaka maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Hii ni kwa sababu Mungu ni upendo unaowaambata watu wote kwani wote wametenda dhambi na kutindikiwa neema na kwamba, upendo wa Mungu hauna mipaka unawakumbatia na kuwaambata wote.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu ameonesha upendo wa hali ya juu kwa kuwaosha mitume wake miguu kazi ambayo kimsingi ilikuwa inatekelezwa na watumwa kama kielelezo cha ukarimu kwa wageni. Yesu anageuza kibao cha maana hii na kuifanya ile kazi ya watumwa, kiasi cha kumshtua Mtakatifu Petro ambaye alitaka kumkataza Yesu asimwoshe miguu! Yesu anachukua nafasi hii kuelezea maana ya kitendo kile kuwa ni huduma makini, kielelezo kwamba amekuja ulimwenguni si kwa ajili ya kuhudumiwa bali kuhudumia, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za binadamu. Huu ni upendo usiokuwa na kifani.

Baba Mtakatifu amewaambia wafungwa hawa waliokuwa wanasikiliza mahubiri yake kwa umakini mkubwa kwamba, Yesu Kristo ndiye msingi na kichwa cha Kanisa. Yesu aliwaosha Mitume wake miguu na kwamba, hata yeye anapenda kurudia tena kitendo hiki kwa kuwaosha miguu yao, ili kupandikiza mbegu ya upendo katika maisha yao, kiasi kwamba hata wao wenyewe ndani ya gereza wanaweza kusaidiana kama ndugu wamoja, kwani upendo unamwilishwa katika huduma. Ukuu wa mtu unapaswa kujionesha anasema Baba Mtakatifu Francisko katika huduma kwa watu, hasa zaidi maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Yesu amejinyenyekesha kiasi hata cha kujifanya kuwa mtumwa wa wote, ili kuwakomboa wote wanaogelea katika utumwa wa dhambi na mauti! Yesu anampenda kila mtu jinsi alivyo! Baada ya kuwaosha mitume wake miguu, Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa kuwapatia wafuasi wake: Mkate kuwa ni kielelezo cha mwili wake na Divai, kielelezo cha damu yake azizi. Hivi ndivyo upendo wa Mungu unavyojidhihirisha katika maisha ya wafuasi wake.

Kwa upande wake Nadia Cersosimo, Mkuu wa Gereza la Paliano anasema hili ni gereza maalum sana nchini Italia linalotoa adhabu kwa wahalifu ambao kwa sasa wameamua kushirikiana na vyombo vya sheria ili kuhakikisha kwamba, sheria inashika mkondo wake. Licha ya kuwa ni gereza maalum, lakini majiundo endelevu na katekesi makini vimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza pengo kubwa lililokuwepo kati yao; yamevunjilia mbali kuta za maamuzi mbele na kwamba, kwa sasa wameanza kuonesha mwelekeo mpya kwa kutaka kuandika kurasa mpya za maisha yao.

Gereza hili linahudumiwa kiroho na Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Padre Walter Milandu, Baba wa maisha ya kiroho, Seminari kuu ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu anasema, wamissionari pamoja na waseminari wamekuwa wakitoa huduma ya maisha ya kiroho Gerezani humo kwa katekesi makini pamoja na maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Tukio la Baba Mtakatifu Francisko kutembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya Karamu ya Mwisho, lilipewa uzito wa juu sana na uongozi wa gereza. Wafungwa na Askari magereza, Jumatano tarehe 12 Aprili 2017 walipata nafasi ya kujipatanisha na Mungu na kwamba, maadhimisho haya yamewapatia ari na mwamko mpya katika maisha ya wafungwa na huduma inayotekelezwa na askari magereza. Huu ni mwanzo mpya wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wafungwa na wale wanaowahudumia gerezani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.