2017-04-13 14:52:00

Askofu mkuu Ruwaichi: Tambueni ukuu na utakatifu wa Sakramenti!


Mama Kanisa Alhamisi kuu anaadhimisha mafumbo makuu matatu katika maisha na utume wake: hii ni siku ambayo Kristo Yesu alipoweka rasmi Sakramenti ya Daraja Takatifu ambayo kwayo utume wa Kanisa uliokabidhiwa na Kristo Mitume wake huendelea kutekelezwa katika maisha hadi mwisho wa nyakati: hivyo hii ni Sakramenri ya huduma wa kitume ambayo imegawanyika katika ngazi kuu tatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi.

Kanisa linaadhimisha siku ile iliyotanguliwa kuteswa kwake, Yesu mwenyewe aliweka sadaka ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake Azizi, ili kuendeleza sadaka ya Msalaba hadi atakaporudi kuwahukumu wazima na wafu! Ekaristi ni chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Siku ambayo Yesu aliwaonesha mitume wake upendo usiokuwa na upeo kwa kuwaosha migu yao, changamoto na mwaliko wa kudumisha huduma ya upendo kwa watu wa Mungu, lakini zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali na nafasi zao katika jamii! Kumbe, Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Sakramenti ya Daraja Takatifu ndiyo maana Mapadre wanakusanyika kumzunguka Askofu mahalia ili kurudia tena ahadi zao za Kikasisi pamoja na kubariki Mafuta Matakatifu yatakayotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaadhimisha Alhamisi kuu kwa Mwaka 2017 kwa namna ya pekee kwa kuendeleza maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka wa Padre Kitaifa, Kanisa linapomwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kulizawadia Mapadre wa kwanza wazalendo na tangu wakati huo, kumekuwepo na umati mkubwa wa Mapadre wa Majimbo na Mashirika kutoka Tanzania wanaoendelea kujisadaka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha!

Askofu mkuu Ruwaichi anawataka waamini kuadhimisha Alhamisi kuu kwa mwamko wa pekee kabisa kwa kutambua utakatifu wa Sakramenti ya Daraja Takatifu na Utakatifu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, ambazo kimsingi ni Sakramenti pacha zinazotegemeana na kukamilishana. Waamini wamwombe Mwenyezi Mungu kuishi neema hizi pacha. Kwa wenye Daraja yaani Maaskofu, Mapadre na Mashemasi pamoja na watu wote wa Mungu waishi na kuenzi neema hizi pacha roho ambayo ni stahiki, elekevu na yenye kumrudishia Mungu sifa, shukrani na ukuu, kwa kupania kujitakatifuza kwa kutumia Sakramenti hizi mbili ambazo Kristo Yesu amewaacha wafuasi wake kwa heshima na upendo mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.