2017-04-12 10:22:00

Mshikamano wa Papa Francisko na familia ya Mungu nchini Misri!


Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri kuanzia tarehe 28- 29 Aprili 2017 inaongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri. Baba Mtakatifu anatembelea Misri wakati ambapo bado kuna madonda makubwa yaliyosababishwa na vitendo vya kigaidi ambavyo vimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi. Anakwenda nchini Misri ili kuombea amani na upatanisho wa kitaifa; pamoja na kusaidia kuwarejeshea matumaini watu wanaoishi huko Mashariki ya Kati, ambao kwa miaka mingi sasa wanaishi katika hofu na wasi wasi ya vita.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anasema, mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa nchini Misri yameigeuza Jumapili ya Matawi kuwa ni Jumapili ya mashuhuda wa imani, ambao wamesimama kidete chini ya uongozi thabiti wa Papa Tawadros II ambaye ametaka waamini waliouwawa kikatili kuzikwa Kanisani kama mashuhuda wapya wa imani katika nyakati hizi. Baba Mtakatifu Francisko anakwenda Misri ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani; kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika uekumene wa damu; maisha ya kiroho na sala, lakini zaidi uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Sandri anasema, Makanisa nchini Misri yameendelea kuwa mstari wa mbele katika huduma ya elimu na majiundo makini kwa vijana hasa wale wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini! Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri ni kuendelea kuwatia shime Wakristo nchini humo ambao wanaendelea kuandika historia ya Kanisa kwa njia ya damu yao kama mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ni hija inayopania kuwaunganisha Wakatoliki na Wakoptiki katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Pasaka, changamoto ambayo inavaliwa njuga na Papa Tawadros II.

Ni hija ya kitume inayolenga pia kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hii ni changamoto ya kutambua kwamba, tofauti za kidini na kiimani ni sehemu ya utajiri na urithi wa binadamu unaopaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Waamini wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya imani kwa Mungu mmoja, muumba wa mbingu na dunia, tayari kushikamana kwa ajili ya huduma kwa wote, ili kuwashirikisha wengine huruma ya Mungu. Huruma, haki na amani ni dhana inayowaunganisha waamini wa dini mbali mbali duniani.

Umefika wakati wa kuondokana na misimamo mikali ya kiimani inayopelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao anasema Kardinali Sandri, ili kulinda uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo; kusimama kidete kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wajenge utamaduni wa kushirikiana kwa dhati katika kupambana na changamoto maboleo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, iko siku haki, amani na maridhiano vitaweza kutawala tena nchini Syria, ingawa hadi wakati huu hali ni tete sana kutokana na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Kuna haja ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama wa maisha yao kutoka Iraq. Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Mashariki ya Kati yataendelea kutoa huduma kwa watu wote pasi na ubaguzi.

Kardinali Sandri katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, ukarabati mkubwa uliofanywa kwenye Kanisa la Kaburi Takatifu la Yesu na hatimaye kufunguliwa hivi karibuni ni kielelezo kikuu cha umoja na mshikamano wa Wakristo huko katika Nchi Takatifu. Vatican pamoja na Makanisa mbali mbali yamechangia gharama ya ukarabati wa Kaburi hili kama ilivyojitokeza hata kwa Mfalme wa Yordani. Makanisa mengine ambayo yana umuhimu wa pekee katika historia ya Ukristo yanaendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa. Kardinari Sandri anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchangia kwa hali na mali utunzaji wa maeneo matakatifu. Mchango unaotolewa Ijumaa kuu ni muhumu sana katika huduma za elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni kielelezo cha mshikamano na Wakristo katika Nchi Takatifu. Jitihada zote hizi ni kwa ajili ya utu, heshima na maendeleo ya watu kama ambavyo alikazia sana Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake wa kitume “Populorum progressio” yaani “Maendeleo ya watu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.