2017-04-11 10:03:00

Papa Mstaafu Benedikto XVI: Shuhuda wa imani ya Fumbo la Pasaka!


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, Pasaka ya Mwaka 2017 ina maana ya pekee sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kwani ni siku ambamo anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 90 tangu alipozaliwa! Shuhuda wa kweli wa imani katika Fumbo la Pasaka! Ni tukio la kihistoria linaloonesha uwepo endelevu wa Kristo Mfufuka katika maisha ya Papa Mstaafu Benedikto XVI, kiongozi asiyekuwa na makuu ambaye kwa sasa “amejichimbia katika sala na tafakari” kwa ajili ya Kanisa la Kristo!

Tukio hili limepata uzito wa pekee kwa kuzindia kitabu kinachojulikana kama “Cooperatores veritatis” yaani “Washiriki wa ukweli” ambacho ni mkusanyiko wa nyaraka na machapisho mbali mbali yaliyoandikwa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na utangulizi wake kutolewa na Padre Federico Lombardi, SJ, Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger/BenediktoXVI. Tukio hili limewashirikisha viongozi wakuu wa Kanisa na kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Siku kuu ya Pasaka ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa ni katika Siku kuu hii, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 90 tangu alipozaliwa, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake!

Itakumbukwa kwamba, Joseph Ratzinger alizaliwa tarehe 16 Aprili 1927, ilikuwa ni Jumamosi kuu na kubatizwa, kwenye mkesha wa Siku kuu ya Pasaka kwa Maji mapya ya Kisima cha Ubatizo, huo ukawa ni mwanzo wa mwanga wa imani ya Joseph Ratzinger katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI daima amekuwa anakiri kwamba, tangu mwanzo maisha yake yamefumbatwa katika Fumbo la Pasaka, alama ya neema na baraka katika maisha yake kama Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kwa hakika anasema Kardinali Kurt Koch, hii ni alama ya neema iliyomwezesha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa kweli ni shuhuda wa imani ya Fumbo la Pasaka linalopaswa kutangazwa na kushuhudiwa ili kuonesha ushindi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Ni mwaliko wa kusimama kidete kushuhudia Injili ya upendo dhidi ya chuki, uhasama, kinzani, migogoro na mipasuko ya aina mbali mbali ndani ya jamii na hata wakati mwingine ndani ya Kanisa. Katika tafakari, maisha na utume wake daima amekuwa na utambuzi kuwa ni shuhuda wa imani inayobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka, changamoto kwa waamini kujitahidi kutembea daima katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Itakumbukwa kwamba, mafundisho makuu ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika fadhila kuu tatu: Ukweli, Upendo na Uhuru. Haya ndiyo mambo makuu yanayojitokeza katika Nyaraka zake za kitume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwanadamu anaweza kuwa na furaha ya kweli ikiwa kama ndani mwake kuna ukweli na upendo na kwamba ukweli unamweka mtu huru kabisa! Hakuna mgogoro wala ukinzani kati ya upendo na ukweli, bali fadhila hizi kuu tatu zinategemeana na kukamilishana katika maisha ya mtu! Upendo pasi na ukweli unageuka kuwa ni giza totoro! Na ukweli pasi na upendo unageuka kuwa ni ukatili. Maisha ya Kikristo yanabubujika kutoka katika upendo wa Mungu kwa waja wake, changamoto na mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema anasema Kardinali Kurt Koch kumwilisha upendo katika uhalisia wa maisha ya watu wanaowazunguka!

Upendo wa Kristo unawawajibisha waamini na kamwe si kama maji kwa glasi! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amechangia kwa kiasi kikubwa mchakato wa upyaisho wa mafundisho Tanzu ya Kanisa Katoliki. Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki ni matunda ya juhudi zake katika kazi ya kuhariri na leo hii ni muhtasari wa kile ambacho Kanisa lina: amini, adhimisha, ishi na kusali! Amewasaidia watu kufahamu maana ya Kanisa, umuhimu wa imani ya Kikristo na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda. Imani ya Kikristo ni zawadi kwa mtu binafsi, lakini inayomwilishwa na kushuhudiwa katika maisha ya Jumuiya ya Kanisa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema amezaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu katika Familia kubwa ya watu wa Mungu, kielelezo cha zawadi, huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.