2017-04-11 14:48:00

Baraza la Makardinali kuchambua majina ya watakatifu wapya!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 20 Aprili 2017 ataongoza Kikao cha kawaida cha Baraza la Makardinali sanjari na Ibada ya Masifu ya Adhuhuri ili kupitisha majina ya Wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Watakatifu; kati yao ni Watoto wa Fatima yaani: Francis na Yacina Marto, ambao kwa mwaka 2017, Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea huko Fatima na kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 12 -13 Mei 2017 kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko.

Wengine wanaotarajiwa kutangazwa kuwa Watakatifu ni Andrea de Soveral, Ambrogio Francesco Ferro, Padre wa Jimbo; Matteo Moreira, mwamini mlei pamoja na wenzao 27 mashuhuda wa imani. Wengine katika orodha hii ni Cristoforo, Antonio na Giovanni, watoto mashuhuda wa imani. Padre Faustino Miguez, mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Calasanzi wa Mchungaji mwema. Orodha hii inapambwa na uwepo wa Padre Angelo da Acri, Mkapuchini. Taarifa hii imetolewa na Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Majigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.