2017-04-10 10:47:00

Papa Francisko asema, sayansi na teknolojia ni kwa ajili ya watu!


Tume ya Taifa ya Usalama wa Kibayolojia, Bioteknolijia na Sayansi ya Maisha nchini Italia, inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, chini ya usimamizi wa Baraza la Mawaziri nchini Italia. Tume hii inakabiliwa na tema tete na zenye umuhimu wa pekee katika maisha ya watu katika ulimwengu mamboleo; kama mtu binafsi mintarafu mahusiano yake na jamii kwa kuanzia katika ngazi ya familia, jumuiya mahalia, kitaifa na kimataifa kama sehemu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu na kumweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa dhati na Tume hii ya Kitaifa katika maeneo ya sayansi na teknolojia ya maisha ili kuwezesha maisha yaweze kukua na kuongezeka, kuzaa matunda kadiri ya tunza ya binadamu aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu: Mwanadamu anahimizwa na Maandiko Matakatifu kulinda bustani ya dunia, maana yake ni kuilinda, kuitunza, kuiendeleza pamoja na kuidumisha.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 10 Aprili 2017 kwa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Usalama wa Kibayolojia, Bioteknolijia na Sayansi ya Maisha nchini Italia alipokutana nao mjini Vatican. Amewakumbusha kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kusongezesha mbele uwiano bora katika matumizi bora ya tafiti za kisayansi na kiteknolojia mintarafu mchakato wa kibaolojia wa viumbe hai, kwa kuwa makini kuangalia matokeo hasi yanayoweza kusababishwa na matumizi potofu ya maarifa na ujuzi unaoweza kupotosha maisha ya viumbe hai.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwanayasansi na fundi wanapaswa “kufahamu” pamoja na “kufahamu kutenda”  kwa umakini mkubwa katika maeneo yao ya kujidai, kwa kufanya maamuzi yanayowajibisha, tayari kusimama na kutafakari, kuamua na kufuata njia nyingine ambayo ni bora zaidi kwa kuongozwa na kanuni ya uwajibikaji muhimu sana katika utendaji wa binadamu mintarafu utekelezaji wa matendo yake au kushindwa kutekeleza, kwa kujihoji binafsi na mbele ya wengine na hatimaye, mbele ya Mwenyezi Mungu.

Teknolojia na maendeleo ya sayansi yanampatia binadamu uwezo mkubwa na hatari yake kwa wananchi wa kawaida na Serikali katika ujumla wake, hawana uwezo wa kutambua kwa haraka utata na changamoto zake; masuala mtambuka yanayopaswa kuvaliwa njuga pamoja na hatari ya kutumia vibaya nguvu ya sayansi na maendeleo ya teknolojia yaliyomo mikononi mwa binadamu! Baba Mtakatifu anasema, pale ambapo teknolojia na faida kubwa vinasigana, maisha ya binadamu na mielekeo ya mafungamano ya kijamii inaweza kujikuta imeelemea zaidi katika ukuaji wa viwanda na biashara kwa hasara na maporomoko ya wananchi na mataifa maskini zaidi duniani. Si rahisi kuweza kupata uwiamo bora zaidi katika masuala ya kisayansi, uzalishaji, kanuni maadili, kijamii, kiuchumi na kisiasa ili kusongezesha mbele mchakato wa maendeleo endelevu yanayoheshimu na kulinda mazingira nyumba ya wote. Ili kupata mwelekeo wa namna hii kuna haja ya kuwa na unyenyekevu, ujasiri, uwazi katika majadiliano na mielekeo mbali mbali ya maisha kwa kuwa na uhakika kwamba ushuhuda uliotolewa na wanasayansi kuhusu ukweli na mafao ya wengi yatasaidia kukuza uelewa wa wananchi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewakumbusha wajumbe wa Tume hii kwamba, sayansi na teknolojia imewekwa kwa ajili ya binadamu na ulimwengu na wala si kinyume chake yaani binadamu na ulimwengu kwa ajili ya sayansi na teknolojia. Mambo haya mawili yanapaswa kusaidia maboresho ya maisha ya binadamu kwa sasa na kwa siku za usoni, kwa kuitengeneza dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi na kwa mshikamano, kwa kuilinda na kuitunza! Baba Mtakatifu amewatia shime wajumbe wa Tume hii kuhakikisha kwamba, wanaenzi mchakato wa maelewano kati ya wanasayansi, mafundi, wafanyabiashara pamoja na wawakilishi wa taasisi mbali mbali kutambua mikakati mbali mbali tayari kujikita katika uragibishaji wa maoni ya jamii yanayopatikana kutokana na maendeleo ya sayansi ya maisha na bioteknolojia.

Na Padre Richard  A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.