2017-04-08 14:34:00

Maadhimisho ya Juma Kuu katika maisha ya Wakristo!


Jumapili ya Matawi, Familia ya Mungu inamshangilia Kristo Yesu anapoingia mjini Yerusalemu kama Mfalme na Masiha, huku watoto wa Wayahudi wakitandaza nguo zao njiani! Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Juma kuu, ambamo Mama Kanisa anaadhimisha Mafumbo makuu ya Kanisa yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kiini cha imani na matumaini ya Kanisa. Kristo Yesu kwa njia ya utii wake anatimiza sadaka yake Msalabani.

Kimsingi, Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Siku ile Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Daraja Takatifu na kuwapatia wafuasi wake kielelezo na mfano bora wa kuigwa katika upendo unaomwilishwa katika huduma makini, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Ijumaa Kuu, Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu kilichosababishwa na dhambi za binadamu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Jumamosi kuu, ni kipindi cha Mkesha, tayari kuadhimisha Siku kuu ya Pasaka, yaani Ufufuko wa Kristo Yesu, kutoka kwa wafu!

Askofu mkuu Paolo Pezzi wa Jimbo kuu la Moscow, Russia anawakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, imekuwa ni nafasi ya kutafakari na kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Maadhimisho ya Juma Kuu, linalotawaliwa na kimya kikuu ni wakati muafaka wa kuchunguza ni mambo yepi ambayo yameacha chapa ya kudumu katika maisha yao baada ya maadhimisho ya Mwaka wa  huruma ya Mungu.

Waamini wawe na ujasiri wa kujiuliza ni mambo yepi ambayo yamegeuka katika maisha yao baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu? Majibu ya maswali haya msingi yatawasaidia waamini kujiandaa na hatimaye, kuadhimisha vyema Fumbo la Pasaka kwa Mwaka 2017. Hivi ndivyo Askofu mkuu Paolo Pezzi anavyoandika katika barua yake ya kichungaji wakati wa Juma kuu kama sehemu ya maandalizi ya Siku kuu ya Pasaka. Ni wakati muafaka kwa kila mwamini kujiuliza dhamana na utume wake katika Kanisa ni upi? Mchango wake katika maboresho ya ulimwengu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi ni upi?

Askofu mkuu Paolo Pezzi anasema, upendo na huruma ya Mungu inashuhudiwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu ameshinda dhambi na mauti, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Anapenda kuchukua nafasi hii kuwaalika waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Juma kuu, ili waweze kufuata Njia ya Msalaba, kuteswa, kufa na hatimaye, kufufuka pamoja na Kristo, tayari kutembea katika mwanga mpya wa maisha. Juma kuu ni kipindi cha kuonesha, umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa. Waamini wajitahidi kuwa ni: mikono, miguu na sauti ya Kristo katika huduma kwa jirani zao, lakini zaidi kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni mashuhuda amini wa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.