2017-04-07 14:50:00

Watanzania wametakiwa kudumisha na kuenzi muungano!


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaomba viongozi na wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha na kuulinda Muungano ulioachwa na waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Ametoa kauli hiyo Ijumaa, Aprili 7, 2017 mara baada ya kushiriki hitma na kuzuru kaburi la Sheikh Karume lililoko Afisi Kuu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui mjini Unguja wakati wa maadhimisho ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Sheikh Abeid Karume sambamba na siku ya Mashujaa Zanzibar Amesema ni muhimu kwa wananchi kutenga muda wao na kuwaombea viongozi wetu waliotangulia mbele ya haki, lengo likiwa ni kukumbuka na kuenzi mchango mkubwa waliotoa katika kujenga msingi wa maendeleo ya Taifa. Waziri Mkuu amesema Watanzania wote Bara na Visiwani ni wamoja kiasili, hivyo wanapaswa kushirikiana katika kudumisha misingi iliyoachwa na waasisi wa Taifa ili kuweza kujiletea maendeleo

Pia amewaomba Watanzania wote kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja kuulinda na kuudumisha Muungano ulioachwa na waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Karume. “Tuhakikishe Muungano huu tulioachiwa na wasisi wa Taifa letu unadumu ili tuendelee kuwa wamoja na kuzungumza lugha moja ya kuboresha maendeleo na kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” amesema. Aidha, Waziri Mkuu amesema katika kutambua umuhimu wa viongozi hao Serikali imetenga siku maalumu kwa ajili ya maadhidhimisho ya vifo vya viongozi hao na kutoa fursa kwa wananchi kila mtu kwa imani yake kuwaombea dua na kutafakari namna walivyojitoa kwa taifa letu.  Maadhimisho ya kifo cha Sheikh Karumbe ni Aprili 7 ya kila mwaka na Hayati Mwalimu Nyerere ni Oktoba 14 ya kila mwaka.

Maadhimisho hayo ya kifo cha Sheikh Karume yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd. Wengine ni Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Sheikh Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Gharib Bilal, wazee wa CCM pamoja na wananchi.

Wakati huo huo, WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Viettel ya Vietnam inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini ambao umefanikisha kuweka miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417 nchini Tanzania Amesema mradi huo ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2015-2017, umewezesha pia ofisi za Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya 131 na Ofisi za Posta 68 kufikiwa na mtandao huo. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Alhamisi, Aprili 6, 2017 Bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake ukiwemo Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018

Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; Mradi wa Anuani za Makazi na Postikodi; na kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji wa huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na huduma za kibenki. “Sekta ya mawasiliano inatekeleza Programu ya Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school), Mradi wa Video Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika mikoa 26 na taasisi za Serikali,” amesema. Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuhifadhi taarifa na mifumo ya Serikali (Government Data Centre) ambacho lengo lake ni kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa unaoenda sambamba na uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu amesema Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kujenga uchumi wa viwanda, na kwamba inatoa kipaumbele kwenye viwanda vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini, vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa nchini na nje ya nchi. “Katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa nchini pamoja na mashirika ya umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza na kujenga viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali nchini,” amesisitiza.  Ameyataka mashirika ya umma yahakikishe kwamba mipango yao inaendana na utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni kujenga uchumi wa viwanda.

Akizungumzia kuhusu juhudi za Serikali kupambana na rushwa, Waziri Mkuu amesema Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina mzaha wala uvumilivu na vitendo vya rushwa. “Hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba, 2015 zimetambuliwa na mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa duniani. Taarifa ya Shirika la Transparency International kwenye utafiti wake kuhusu mtazamo wa rushwa mwaka 2016, imeonesha kuwa viwango vya rushwa vinaendelea kupungua hapa nchini,” amesema. Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali iliweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.75 kutokana na operesheni zilizofanywa na TAKUKURU,

“TAKUKURU imefanya uchunguzi wa majalada 306 ya tuhuma za rushwa na kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kuendelea na mashtaka kwa majalada 104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU iliendesha kesi 674 zikiwemo kesi mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407 zinaendelea kusikilizwa mahakamani,” amesema. Katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaendelea na mapambano dhidi ya rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali, kudhibiti matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi mabaya ya fedha za ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imefungua balozi mpya sita katika nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki. Amesema Balozi hizo zina kazi ya kuendeleza juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi vya utalii na rasilimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo ikizingatiwa utulivu na amani iliyopo nchini Tanzania.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.

Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.