2017-04-05 07:02:00

Papa Francisko akutana na Mtoto wa Mfalme Charles na mke wake Camilla


Baba Mtakatifu Francisko Jumanne jioni, 4 Aprili 2017 amekutana na kuzungumza na Mtoto wa Mfalme Charles pamoja na mke wake Camilla ambao baadaye walipata pia nafasi ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenye Ukumbi mdogo wa Paulo VI mjini Vatican. Hii ni mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na Mtoto wa Mfalme pamoja na mke wake ambao kwa sasa wako nchini Italia kutembelea hasa zaidi maeneo yaliyoathirika kwa tetemeko la ardhi kama kielelezo cha upendo na mshikamano na wahanga wa majanga haya ya asili.

Baba Mtakatifu pamoja wageni wamegusia kwa namna ya pekee watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na baa la umaskini linaloendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Baada ya mazungumzo yao ya faragha Baba Mtakatifu na wageni wake walibadilishana zawadi.  Mtoto wa Mfalme Charles pamoja na ujumbe wake, wamebahatika pia kutembelea “Hifadhi za Nyaraka za Siri za Vatican” pamoja na Maktaba kuu ya Vatican ambako wamejionea wenyewe baadhi ya Nyaraka muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Mtoto wa Mfalme pamoja na ujumbe wake, walipata nafasi pia ya kusalimiana na wafanyakazi wa Vatican kutoka Uingereza na baadaye, kukutana pia na Jumuiya ya Waingereza wanaoishi mjini Roma, kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mwenyeheri Beda, hapa Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.