2017-04-03 14:00:00

Papa Francisko: biashara haramu ya binadamu ni kashfa ya kimataifa!


Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inakomesha biashara haramu ya binadamu inayoendelea kuwatumbukiza watu katika utumwa mamboleo, nyanyaso na ukiukwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Mkutano wa 17 wa Mshikamano dhidi ya biashara haramu ya binadamu ulioandaliwa na Shirikisho la Ushirikiano Kimataifa, Usalama na Maendeleo, OSCE unaofanyika mjini Vienna, nchini, Austria.  Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umesomwa kwa niaba yake na Padre Michael Czerny, Katibu mkuu Msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuonesha utashi wa kisiasa katika kupambana ili hatimaye, kung’oa kabisa biashara haramu ya binadamu duniani, kielelezo cha uhalifu mkubwa dhidi ya utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Hii ni biashara ambayo inaendelea kushika kasi sehemu mbali mbali za dunia, biashara ambayo inapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa mkutano huu kujizatiti kikamilifu katika kuendeleza mchakato wa uragibishaji wa janga hili dhidi ya utu wa binadamu, ili kuokoa maisha ya watoto wengi wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu. Ni dhamana kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya binadamu inadhibitiwa kikamilifu na hatimaye, kukomesha hata utumwa mamboleo. Biashara hii inaendelea kushamiri na kuota mizizi hata kwenye Nchi wanachama wa OSCE anasikitika kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa upande wake Padre Michael Czerny, ameshirikisha mbinu za kuweza kuzuia watoto na watu wazima kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu kwa kuzingatia: kanuni maadili na utu wema, Utawala wa sheria; kwa kuwekeza katika elimu makini, mapambano dhidi ya umaskini na maradhi. Amekazia umuhimu wa kuwalinda watoto hasa: wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wanaojikuta wametumbukizwa katika misafara ya wakimbizi na wahamiaji. Watoto hawa wapewe makazi, huduma ya afya, elimu na kazi kwa wakati wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa.

Dhuluma na nyanyaso mbali mbali zimepelekea makundi makubwa ya watoto na watu wazima kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu, kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na sanjari na kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wote ili mkondo wa sheria uweze kufanya kazi yake. Rushwa inapaswa kudhibitiwa katika vyombo vya sheria. Mshikamano utaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa: kuzuia, kulinda na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Serikali na viongozi wa kidini wakishirikiana kwa dhati, janga la biashara haramu ya binadamu linaweza kupewa kisogo. Mchakato huu unawezekana kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kujadiliana; kwa kudumisha mafungamano ya kijamii; kwa kuvishirikisha vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Baba Mtakatifu anasema, watoto ni alama ya matumaini na maisha; kielelezo cha jamii, kumbe wanapaswa kupokelewa, kupendwa, kutunzwa na kulindwa! Pale ambapo familia ni madhubuti, hata Jamii pia inaimarika na kujikita katika utu wema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.