2017-04-03 13:45:00

Papa Francisko aunda Majimbo mapya mawili na kuteuwa Maaskofu wake!


Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzingatia mahitaji ya shughuli za kichungaji ameamua kuunda majimbo mawili yaani Jimbo Katoliki la Evinayong na Mongomo yanayounda Jimbo kuu la Malabo huko Guinea Equatorial na kuteuwa Maaskofu wake wa kwanza kuwa ni Calixto-Paulino Esono Abaga Obono kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Evinayong na Padre Juan Domingo-Beka Esono Ayang kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Mongomo. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Padre Miguel Angel Nguema Bee kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Ebebiyin, Equatorial Guinea.

Askofu mteule Calixto-Paulino Esono Abaga Obono wa Jimbo Katoliki la Evinayong, alizaliwa kunako tarehe 17 Machi 1969 huko Ebang-Zomo Ebebiyin. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi kunako tarehe 22 Desemba 2000 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kwa muda wote huo amekuwa Paroko na kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2005 alipelekwa na Jimbo kwa ajili ya kujiendeleza zaidi huko Navarra, Hispania. Kuanzia mwaka 2005 hadi anateuliwa kuwa Askofu alikuwa ni Paroko na Gombera wa Seminari Ndogo ya Juan Pablo II huko Bata na Mkurugenzi wa Idara ya Afya Kijimbo.

Askofu mteule Juan Domingo-Beka Esono Ayang wa Jimbo Katoliki Mongomo alizaliwa kunako tarehe 18 Februari 1969 huko Mabewele- Yenkeng, Bata. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadre tarehe 2 Septemba 2002 akaweka nadhiri za daima na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 28 Septemba 2003. Tangu wakati huo amekuwa ni Mkurugenzi wa Chuo cha Mapadre wa Claret na Paroko usu wa Parokia ya Maria Reina. Kuanzia mwaka 2004 – 2008 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Chuo cha Waclaret huko Luba na Paroko usu Parokia ya Nuestra Senora de Monserrat. Mwaka 2008 – 2014 aliteuliwa kuwa Paroko wa Madhabahu ya Waclaret huko Malabo. Kati ya Mwaka 2014 – 2016 alipelekwa na Jimbo kwa masomo ya juu nchini Hispania. Tangu Mwaka 2016 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu alikuwa ni Mchumi wa Seminari kuu ya Waclaret “La Purisima” mjini Bata na amekuwa pia ni Jaalimu katika taasisi mbali mbali za elimu nchini humo!

Askofu mteule Miguel Angel Nguema Bee wa Jimbo Katoliki Ebebiyin, Equatorial Guinea alizaliwa 13 Julai 1969. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadre tarehe 9 Julai 1998 akaweka Nadhiri za Daima na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre 24 Julai 2000. Kati ya mwaka 2000 – 2004 alikuwa anashiriki kat8ika utume kwenye Jumuiya ya Wasalesiani iliyoko Pointe Noire na kusaidia kama Mchumi wa Jumuiya. Mwaka 2004 – 2008 akateuliwa kuwa Mkuu wa Jumuiya ya Kanda ya Youndè, nchini Cameroon. Kunako mwaka 2014 akateuliwa kuwa Mkuu wa Kanda ya Equatorial Afrika kwa awamu mbili, hadi alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Ebebiyin, Equatorial Guinea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.