2017-04-03 13:27:00

Askofu mkuu Giacomo Ottonello ateuliwa kuwa Balozi nchini Slovakia


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Giacomo Guido Ottonello, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Slovakia. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Ottonello alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Equador. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Giacomo Guido Ottonello alizaliwa kunako tarehe 29 Agosti 1946 huko Masone, nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Juni 1971 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Kunako tarehe 29 Novemba, akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na kumweka wakfu tarehe 6 Januari 2000 wakati, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo sanjari na Siku ya Tokeo la Bwana. Tangu alipoteuliwa kuwa Askofu mkuu ametekeleza dhamana na wajibu wake kama Balozi wa Vatican huko Panama, Equador na sasa ameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kumwakilisha nchini Slovakia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.