2017-04-02 15:03:00

Ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati ni vinasaba vya watu wa Carpi!


Askofu Francesco Cavina wa Jimbo Katoliki la Carpi, Italia, Jumapili tarehe 2 Aprili 2017 mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Mashuhuda Jimbo Capri, ametumia nafasi hii kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea na kuwatia shime katika shida na mahangaiko yao baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi kunako mwaka 2012. Amewashukuru wadau mbali mbali ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanafanikisha hija ya Baba Mtakatifu Francisko Jimboni mwao.

Amemshukuru pia Papa Mstaafu Benedikto XVI kwa uwepo na msaada wake wa daima katika sala. Kanisa kuu la Bikira Maria Mpalizwa mbinguni, linalojulikana pia kama “Kanisa dogo la Mtakatifu Petro” linaonesha uhusiano wa dhati kati ya familia ya Mungu Jimboni Carpi na Vatican katika ujumla wake. Hapa ni eneo la wachapakazi, watu wanaoshirikiana na kushikamana; watu ambao umoja, ukarimu na upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha yao ya kila siku! Hizi ni tunu msingi ambazo zimekuwa ni chachu ya mafungano ya kikanisa na kijamii Jimboni Carpi.

Ni fadhila hizi ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha zoezi zima la ujenzi na ukarabati wa miundo mbinu ya eneo hili baada ya kupigiswa magoti na tetemeko la ardhi! Hii ndiyo changamoto na mwaliko kwa waamini kujibidisha kukutana upya na Kristo Yesu katika historia na maisha yao, tayari kushuhudia furaha ya kukutana na Yesu katika maisha yao, tayari kushuhudia utu mpya unaoweza kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidugu na ukombozi wa kweli.

Hivi ndivyo walivyoshuhudia watu kama: Mtakatifu Bernadino Realino, aliyejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu kama Myesuiti. Hawa ni watu kama Padre Zeno Saltini, Mama Ninna, Mwalimu Albertina Violi pamoja na Shuhuda wa imani Odoardo Focherini, mwenye haki kati ya watu wa mataifa! Hili ni eneo ambalo daima limesimama kidete kulinda na kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo hata wakati wa madhulumu ya kinazi. Carpi ni mji ambao umeonesha ukarimu kwa wafungwa kwa kuwasaidia kiroho na kimwili chini ya uongozi wa Padre Francesco Venturelli. Uwepo wa watu wengi katika eneo hili ni ushuhuda kwamba, maisha yatashinda daima!

Askofu Francesco Cavina anakaza kusema haya ni maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Yesu anayewaondolea woga na wasi wasi katika maisha kwa kutambua kwamba, daima yuko pamoja nao, Kanisa na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anaonesha dira na njia ya kufuata na baada ya maisha haya ya hapa duniani, kuweza kupata maisha ya uzima wa milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.