2017-04-02 15:17:00

Papa Francisko: Mapadre jisadakeni kujibu kilio cha maskini!


Chuo Kikuu cha Kipapa cha Kihispania cha Mtakatifu Yosefu kilichoko mjini Roma, tarehe 1 Aprili 2017 kimeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 125 tangu kuanzishwa kwake kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewataka Mapadre wanaofundwa chuoni hapo kuondokana na dhana ya Upadre kama ajira na badala yake, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hata ikibidi kuuza mavazi yao kwa ajili ya kujibu kilio cha maskini! Chuo hiki kilianzishwa na Mwenyeheri Manuel Domingo y Sol, Muasisi wa Chama cha Udugu wa Mapadre wa Jimbo wa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa mambo makuu matatu: Kupenda kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili zako zote, sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Marko 12: 30. Kupenda kwa moyo wako wote anafafanua Baba Mtakatifu kwa kusema ni hali ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma pasi na kutafuta masilahi, ustawi au mafao binafsi kwa kujikita katika upendo wa kichungaji ili kuwafahamu, kuwapenda, kuwapokea, kuwasamehe kwa moyo wote na kuwahudumia wengine mintarafu kifungo cha shughuli za kichungaji.

Mchakato huu unatekelezwa ndani ya Jumuiya inayounganishwa na kifungo cha upendo kati ya Mapadre kwa ajili ya huduma ya kichungaji inayojikita katika udugu; dhamana inayohitaji kwa kiasi kikubwa uwepo wa Roho Mtakatifu ili  kuendeleza mapambano binafsi ya maisha ya kiroho, changamoto endelevu hata katika ulimwengu mamboleo, ili kuvuka ubinafsi; kwa kukumbatia utofauti kama sehemu ya utajiri wa umoja na mshikamano kati ya Mapadre, alama makini ya uwepo wa Mungu katika maisha ya Kijumuiya. Uwepo huu unashuhudiwa wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, alama ya upendo wa Mungu katika nyoyo za Mapadre wake.

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kupenda kwa roho yao yote, maana yake ni kuwa tayari kujitoa bila ya kujibakiza hata kama ikibidi kufa, ushuhuda ambao umetolewa na Mwenyeheri Manuel Domingo. Kumbe, majiundo ya Kikasisi hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa elimu dunia, lakini hii ni sehemu ya mchakato unaojumuisha maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Malezi na majiundo ya Kikasisi ni hatua muhimu sana inayowasogeza Majandokasisi kwa Mungu na jirani kwa kujikita katika mang’amuzi yanayofanywa kwa msaada wa Roho Mtakatifu katika sala endelevu. Kwa njia hii hata Mapadre wanaweza kushiriki vyema kuwaunda na kuwafunda wengine. Majiundo ya Kikasisi yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika mihimili ya: kiakili, kiroho, kijumuiya na katika shughuli za kitume, kiasi kwamba, kunakuwepo na mwingiliano wa dhati. Pale panapokosekana moja ya mihimili hii ya majiundo, Mapadre wanaanza “kuchechemea na hatimaye kugeuka viwete katika maisha na utume wao”!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kupenda kwa akili zako zote ni kuonesha vipaumbele, amana na hazina ya maisha yako badala ya mtu kutafuta uhakika na usalama wa maisha kwa mambo mpito ambayo wakati mwingine yanawatumbukiza na hatimaye, kumezwa na malimwengu! Mapadre wajenge moyo wa kuwa na kiasi, kwa kuambata ufukara kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na Kristo Yesu ambaye alikuwa tajiri katika yote lakini akaacha yote na kuambata umaskini kwa ajili ya upendo kwa waja wake. Baba Mtakatifu anawaonya Mapadre wasipende sana fedha na badala yake wajenge na kukuza utamaduni wa shukrani kwa wema na ukarimu wa Mungu katika maisha yao! Wawe tayari kujinyima na kujisadaka kwa ajili kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama mashuhuda amini wa Kristo Yesu katika mchakato wa kudumisha haki jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.