2017-04-02 14:40:00

Papa Francisko aguswa na mateso ya watu: DRC, Paraguay na Venezuela


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Mashuhuda Jimbo Katoliki la Carpi, Jumapili tarehe 2 Aprili 2017 anasema kwamba, anasikitishwa sana na taarifa ya mapigano yanayoendelea mkoani Kasai, nchini DRC; mapambano ya silaha yanayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna makundi makubwa ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao na kwamba, viongozi na mali za Kanisa nazo zinaendelea kuharibiwa vibaya na mapigano haya.

Baba Mtakatifu anapenda kuchuku fursa hii kuwahakikisha wote hawa, uwepo wake wa karibu na anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini DRC, ili kweli mioyo ya watu hawa wanaovuruga amani iweze kutubu na kumwongokea Mungu badala ya kuendelea “kuogelea” katika chuki na mapigano!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, anafuatilia kwa umakini mkubwa yale yanayoendelea kutukia nchini Venezuela na Paraguay. Anasali ili kwamba, mataifa haya mawili ambayo anayapenda kwa namna ya pekee kuachana na kinzani na badala yake waendelee bila kuchoka wala kukata tamaa katika kutafuta suluhu ya kisiasa katika migogoro na kinzani zilizopo!

Baada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu amewaalika waamini kumshukuru na kumtolea Bikira Maria: furaha, mateso na matumaini yao: wamwombe ili aweze kuwaangalia kwa jicho la huruma wale wanaoteseka hasa zaidi wagonjwa, maskini na watu wasiokuwa na ajira. Mwenyeheri Odoardo Focherini na Mtumishi wa Mungu Marianna Saltini, mashuhuda wa upendo wa Kristo, wawe kwao ni mfano bora wa kuigwa. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano na viongozi wa Kanisa, daima wakilenga katika mambo msingi ya maisha kwa kutangaza na kushuhudia Injili. Wakleri wajitajidi kuwa karibu na waamini wao na mwishoni, amewashukuru wote waliosaidia kuandaa na hatimaye kuwezesha kufanikisha ziara yake Jimboni Carpi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.