2017-04-02 15:35:00

Dhamana na wajibu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki!


Ili kuweza kufundisha na kurithisha elimu, ujuzi na maarifa kwanza kabisa kuna haja ya kujifunza kwa makini. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliomwandikia Kardinali Giuseppe Versaldi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Perù, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa chuo hiki ambacho kwa hakika kimekuwa ni chemchemi ya huduma kwa familia ya Mungu nchini Perù.

Baba Mtakatifu anasema, maadhimisho haya ni nafasi ya kutafakari kwa makini asili na lengo la elimu inayotolewa Chuo Kikuu cha Kikatoliki, kinachoundwa na Jumuiya ya walimu, wanafunzi na wafanyakazi wanaojisadaka kwa ajili ya elimu na maisha! Jambo la msingi linalotiliwa mkazo ni Jumuiya inayoshikamana na kutembea kwa pamoja; tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kurithisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu, kijamii na kitamaduni kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, waweze kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na Jamii ya Perù katika ujumla wake.

Huu ni mwaliko wa kuwa wazi kwa tamaduni nyingine zinazowazunguka ili kutajirishana kwa njia ya majadiliano ya kina! Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, hii ni Jumuiya ambayo kila mtu anawajibu na dhamana amabyo anapaswa kuitekeleza kama njia ya kukamilishana, kwa kutambua kwamba, Mwalimu wao ni mmoja tu naye ni Kristo Bwana, wanayepaswa kufuata nyayo zake, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, dhamana inayotekelezwa kwa uvumilivu na unyenyekevu, daima wakijitahidi kujenga uhusiano wa karibu na Yesu.

Ili kuweza kufundisha kwa dhati kwanza kabisa kuna haja ya kujifunza, kwani mwanafunzi ni yule ambaye anafuata nyayo na mafano wa mwalimu wake, makini katika mafundisho ili aweze kuyaboresha na ikiwezekana kumpita hata mwalimu wake, hali inayowafanya wadau mbali mbali katika elimu kuwa wanyenyekevu na watu wanaohitaji neema na baraka ya Mungu katika maisha yao, ili kuweza kutumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Kufundisha na kujifunza ni mchakato unaokwenda taratibu sana katika maisha, lakini muhimu katika ujenzi wa upendo na ushirikiano na Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, kusaidia kukamilisha kazi ya uumbaji.

Dhamana hii takatifu anasema Baba Mtakatifu Francisko inasaidia kufahamu na kuboresha wema uliomo ndani ya kila kiumbe kwani kinaakisi na kupendwa na Mungu. Kutokana na dhamana hii, Jumuiya ya Chuo kikuu inategemeana na kukamilishana, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake; kwa kutambua wito na mwelekeo wa maisha yake ili Chuo kikuu kiweze kupeta na kung’ara si tu kitaaluma, bali kama shule ya utu wema! Lengo la Chuo Kikuu cha Kikatoliki ni kusaidia kuwafunda wainjilishaji na wainjilishwaji, ili kwa kukutana na Kristo Bwana, waweze kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika uhalisia na vipaumbele vya watu, kielelezo cha Injili hai kati ya walimwengu, ili watu kwa kuona mifano bora ya maisha, waweze kumwongokea Mungu na hivyo kuwa ni viumbe wapya!

Chuo Kikuu cha Kipapa cha Kikatoliki Perù hakina budi kujizatiti ili kuweza kukabiliana na hatimaye, kujibu changamoto za watu wa nyakati hizi, kwa kuwapatia neno la kweli na yenye uhakika; kwa kujikita katika ukweli angavu ili kuutangaza kwa kushirikiana na watu wote na jamii katika ujumla wake. Asili, historia na utume wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Perù ina onesha mafungamano ya pekee na Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa la Kiulimwengu na kwamba, Chuo hiki kinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa weledi katika maisha ya binadamu kwani kimsingi Mkristo anapaswa kuwa ni shuhuda wa imani na maarifa. Mwishoni, Baba Mtakatifu anaiweka Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Perù chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Kikao cha hekima pamoja na kuendelea kuwakumbuka na kuwasindikiza katika sala zake, wale wote wanaojihusisha na majiundo makini chuoni hapo pamoja na familia zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.